KENYA, SUDAN ZAAHIDI KUSHIRIKIANA KUBORESHA KILIMO

RAIS Uhuru Kenyatta wa Kenya na Kamal Ismael ambaye ni mjumbe maalumu wa Rais wa Sudan Omar Al-Bashir, walifanya kikao cha pamoja Alhamisi katika Ikulu ya Rais jijini Nairobi ili kujadili jinsi wakuimarisha uchumi kati ya mataifa haya mawili.

Viongozi hao wawili waliegemea katika sekta ya zaraa, hasa kukuza miwa itakayounda sukari ya bei nafuu pamoja na kuongeza uuzaji wa chai kutoka Kenya hadi Sudan.

Rais Kenyatta alikariri kuwa aliwahi kujadiliana na Rais al-Bashir kuhusu kukuza miwa ya kuunda sukari ya bei nafuu, ikizingatiwa Sudan hutumia mfumo wa teknolojia ya kisasa kuendesha kilimo cha miwa na kuifanya kuwa na soko bora ya sukari duniani.

"Tunafahamu Sudan ni miongoni mwa nchi zinazokuza miwa kwa kutumia mbinu za teknolojia ya kisasa na kuuza sukari ya bei nafuu katika nchi za kigeni.

Nchi ya Sudan inatambulika kote duniani kutokana na soko bora la sukari, Kenya inapania kuiga mkondo huo," alieleza Rais Kenyatta.

Kadhalika, Rais Kenyatta alisema taifa hili linalenga kujifunza mengi kuhusu kilimo cha pamba kutoka kwa nchi ya Sudan.
Nchi hiyo pia imeimarika katika ukuzaji wa mimea inayounda pamba.
"Kenya ina malengo ya kuunda viwanda vingi vya kutengeneza nguo, hivyo basi ni jambo la busara kuimarisha kilimo cha pamba nchini," alisema.

Novemba 28, 2017 wakati Bw Uhuru Kenyatta na William Ruto wakiapishwa kama Rais na Naibu Rais mtawalia, kuhudumu kwa muhula wao wa pili chini ya serikali ya Jubilee, Rais aidha aliahidi kuegemea katika ajenda nne kuu; Usalama wa chakula na afya bora, makazi nafuu, uundaji wa viwanda na matibabu bora kwa kila mwananchi ili kusongesha mbele taifa hili.

Serikali ya Jubilee imekuwa ikitilia mkazo umuhimu wa zaraa hasa kilimomseto kwa kutumia mbinu za teknolojia ya kisasa kunyunyizia mimea maji ili kukabiliana na uhaba wa chakula nchini.


KENYA, SUDAN ZAAHIDI KUSHIRIKIANA KUBORESHA KILIMO KENYA, SUDAN ZAAHIDI KUSHIRIKIANA KUBORESHA KILIMO Reviewed by KUSAGANEWS on January 25, 2018 Rating: 5

No comments: