Siku 35 baada ya Tundu Lissu kusema mwili wake bado una
risasi moja baada ya kutolewa nyingine 15, jana mbunge huyo wa Singida
Mashariki (Chadema) amelieleza Mwananchi kuwa madaktari wamemtoa kipande cha
risasi kilichokuwa mwilini mwake.
Hata hivyo, mwanasheria huyo mkuu wa Chadema, ambaye
alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 akiwa ndani ya gari lililokuwa nje ya
makazi yake mjini Dodoma Septemba 7 mwaka jana, alisema chuma hicho ni tofauti
na risasi iliyonayo mwilini, ambayo alielezwa na madaktari wa Hospitali ya
Nairobi, Kenya kuwa iko sehemu mbaya, lakini isipotolewa haiwezi kumdhuru.
Jana madaktari wamenitoa kipande cha chuma katika sehemu ya
makalio ambacho nilipokuwa Nairobi (Kenya) madaktari walikiona lakini kilikuwa
ndani ya nyama wakashindwa kukitoa,” alisema Lissu kwa njia ya simu kutoka
Ubelgiji ambako alipelekwa Januari 7 kwa ajili ya tiba ya mazoezi
Kipande hiki kilisogea na wamekitoa. Ni tofauti na ile
risasi ambayo iko mwilini mwangu.”
Akieleza kiundani kuhusu hali yake, Lissu alisema anaendelea
vizuri.
Huu mkono wa kushoto ambao ulikuwa na tatizo, wameunyoosha
na kuufanyia mazoezi kweli kweli na huu mguu wa kulia ambao ndio wenye tatizo,
unaendelea vyema,” alisema.
“Huku ni mazoezi tu. Kwa siku nafanya mazoezi kwa saa nne,
Naingia saa 3:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi, narudi tena saa 5:00 asubuhi
hadi saa 6:00 mchana. Mwisho naingia mazoezini saa 8:00 mchana hadi saa 10:00
jioni. Hiyo ndiyo ratiba yangu kwa siku.”
Alisema katika mazoezi hayo anatumia magongo maalumu pamoja
na kiti cha magurudumu
“Mfano, huu mguu wa kulia natakiwa kuukanyagia kwa kilo 20
hadi 25 katika mzani na mimi nina kama kilo 90. Ninapoukanyagia ninaulizwa kama
unauma, ikiwa sijasikia maumivu ina maana sijafanya kitu, kwa hiyo ni kazi
kwelikweli,” alisema
Kuhusu muda ambao anatakiwa kufanya mazoezi hayo mpaka
atakaporejea katika hali yake ya kawaida, Lissu alisema bado hajajua.
Ah bwana we, hapa madaktari wamegoma kunieleza hilo, lakini
wameangalia katika maungio ya goti la mguu wa kulia kuna mfupa haujaunga
vizuri, ni lini utaunga hilo sijajua,” alisema.
Mara baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi
sasa hawajajulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu
ya awali kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya siku hiyo
usiku.
Desemba 21 mwaka jana wakati akihojiwa na kituo cha
televisheni cha Azam, Lissu alisema madaktari wa Nairobi walimueleza kuwa
risasi iliyokuwa imesalia mwili haina madhara.
Alisema risasi saba zilitolewa na madaktari hao, jambo lililomaanisha
kuwa risasi nyingine nane, zilitolewa na madaktari wa Tanzania, saa chache
baada ya kushambuliwa alipofikishwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Lissu: Nimetolewa ‘risasi’ nyingine mwilini
Reviewed by KUSAGANEWS
on
January 25, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment