JAFO - ZINGATIENI UBORA NA KUEPUKA WAKANDARASI WABABAISHAJI

  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akikagua Barabara za Manispaa ya Kinondoni zinazojengwa kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam mapema leo,

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akikagua ujenzi wa miundombinu katika barabara ya Makumbusho inayojengwa kwa kiwango cha Lami kupitia Mradi wa uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akikagua ujenzi wa barabara ya Makumbusho ambayo inajengwa kwa kiwango cga Lami.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akitoa maelekezo kwa Viongozi na Wataalam wa Manispaa ya Kinondoni baada ya ukaguzi wa miundombinu inayojengwa na mradi wa uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam.
Na Raphael Kilapilo

Waziri  wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Selemani Jafo amewataka wahandisi na watendaji wa Manispaa za Kinondoni, Ilala na Temeke ambazo zinatekeleza Mradi wa Uendelezji Jiji la Dar es Salaam (DMDP), kuzingatia ubora wa hali ya juu katika ujenzi wa miundombinu na kuepuka kujihusisha na wakandarasi wababaishaji.

Waziri Jafo aliyasema hayo wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya DMDP katika Manispaa ya Kinondoni jumatatu tarehe 22 Januari, 2018 na kuwataka wasimamizi hao kutokuwa na mjadala au maafikioano kwenye suala zima la ubora wa barabara.

Akizungumza mara baada ya kukagua Jengo la ofisi za mradi pamoja na barabara za  Makumbusho - Sokoni, Nzasa na Viwandani, Jafo alisema kuwa barabara za DMDP zinazojengwa ni tofauti sana na barabara zilizokuwa zikijengwa awali, zinajengwa kwa ubora wa hali ya juu na zinagharimu fedha nyingi, hivyo hatarajii kuona baada ya muda zinaanza kuharibika.

“Barabara hizi pamoja na miundombinu mingine katika mradi huu katika Manispaa za Dar es Salaa kwa ujumla wake zinagharimu kiasi cha fedha takribani Bil.  660. Hizi ni fedha nyingi, sitarajii kuona baada ya mwaka mmoja au miwili tunaaza kuziba vilaka. Niwatake wahandisi wetu mnaosimamia barabara hizi kuhakikisha zinakuwa na ubora wa hali ya juu uliokusudiwa, hakuna kuafikiana au kukubaliana kuhusu ubora. Fanya mfanyavyo, sihitaji majadiliano kwenye swala la ubora,” alisema Jafo.

Aidha Mhe. Jafo aliwataka uongozi wa Halmashauri hizo kuwaondoa haraka wakandarasi ambao wataonekana kukwamisha utekelezaji au kuharibu kazi.

“ Sitaki utani kwenye ubora na mkibaini mkandarasi anataka kukwamisha kazi hizi kwa njia moja au nyingine aondolewe mapema sana kabla ya kuharibu kazi,” alisema.

Alieleza kuwa nia ya Serikali ni kubadilisha jiji la Dar es Salaam na kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa jiji hilo kwa muda mrefu.

Waziri Jafo alisema kuwa  ataona aibu endapo barabara za jiji la Dar es Salaam zitakosa ubora kama ule ulipo katika barabara za miji ya Tanga, Arusha, Mtwara Mikindani, Kigoma Ujiji, Mbeya, Mwanza na Dodoma ambazo pia zimejengwa kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji Kimkakati (TSCP), unaosimamiwa na OR-TAMISEMI.

Aidha, Jafo alimuagiza Mratibu wa Mradi huo katika Manispaa ya Kinondoni, kukamilisha ujenzi wa jengo la ofisi lenye maabara ya kisasa mapema iwezekanavyo ili alizindue kabla ya Februari 19 mwaka huu.

Pia aliagiza kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Makumbusho-Sokoni  ili nayo iwekewe jiwe la msingi wakati wa uzinduzi wa jengo la Manispaa kuashiria kuanza rasmi kwa utekelezaji wa Mradi wa DMDP unaotarajiwa kimalizika mwaka 2030.

“Tunatoa fedha nyingi sana, lazima kazi hii iende haraka iwezekanavyo. Nataka nije nizundue hili jengo mara baada ya kumaliza Bunge kabla ya February 19 na kuweka jiwe la msingi kwenye hii barabara,” alisema Jafo.

Naye Mratibu wa Mradi wa DMDP wilaya ya Kinondoni, Mkelewe Tungaraza, alimuahidi Mhe. Jafo kuwa, ujenzi wa barabara hizo upo katika hatua nzuri na wataendelea kusimamia kwa karibu ili kuzingatia ubora uliokusudiwa.

Mwisho.


Caption.


2.  
3
4.  


JAFO - ZINGATIENI UBORA NA KUEPUKA WAKANDARASI WABABAISHAJI JAFO - ZINGATIENI UBORA NA KUEPUKA WAKANDARASI WABABAISHAJI Reviewed by KUSAGANEWS on January 24, 2018 Rating: 5

No comments: