Mwanamke Aishia Mikononi mwa Polisi Baada Ya Kukutwa Akifukua Maiti ya Mwanaye........Aliamini Atafufuka Baada ya Siku 3
Mwanamke aliyekuwa akiamini kuwa
mtoto wake angefufuka siku ya tatu baada ya kufariki dunia Februari 15, jana
alizua kizaazaa baada ya kufukua kaburi na kutoa maiti hiyo, hali
iliyosababisha wananchi wafanye vurugu na kuichoma nyumba yake.
Mtoto huyo, Baraka Mwafongo (22),
aliyefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu, alizikwa siku iliyofuata lakini
maiti yake ilifukuliwa usiku wa kuamkia jana na kuwekwa katika pagala ikiwa
imevishwa suti kumsubiri mchungaji aifufue.
Mwanamke huyo, Ruth Segeleti (52),
anayeishi Mtaa wa Shigamba, Mbalizi, hakutaka kuzika maiti ya mwanawe akieleza
kuwa mtoto wake angefufuka baada ya siku tatu, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari.
Alisema polisi waliona kuwa huenda
hana uwezo ndipo walipomsaidia kuzika, lakini usiku wa kuamkia jana alipata
vijana wawili waliomsaidia kufukua kaburi na kuchukua maiti hiyo ambayo
waliipeleka kwenye pagala na kuiweka ikiwa imevishwa suti.
Baada ya wakazi kubaini kaburi la
mtoto huyo limefukuliwa, kundi la watu lilijitokeza makaburini na kusababisha
polisi kufyatua mabonu ya machozi
Wananchi waligundua kuwa kaburi
lilikuwa wazi majira ya saa 3:00 asubuhi baada ya majirani kumuona mwanamke
ambaye walijua alikuwa na msiba wa mtoto wake Jumamosi akiwa na jembe mkononi
na furushi la nguo akitokea makaburini.
“Nilipomsemesha, hakutaka kunijibu,” alisema mkazi wa mtaa huo, Mariam Mwakisepile ambaye ni
jirani wa mwanamke huyo.
“Nililazimika kuwaarifu majirani
wengine ambao walikwenda makaburini ambako walikuta kaburi la Baraka likiwa
limefukuliwa.”
Shuhuda mwingine wa tukio
hilo, Christina Nyopelo alisema walipiga simu kituo cha polisi cha Mbalizi na
kuwaarifu.
“Baada ya muda mfupi polisi
waliwasili na wakiwa makaburini waliona sanduku ndani ya kaburi, lakini mwili
haukuwapo,” alisema Nyopelo.
“Polisi kwa kushirikiana na
wananchi waliamua kukagua maeneo ya makaburi na hatimaye walifanikiwa kuukuta
mwili ukiwa umelazwa kwenye banda lililopo karibu na eneo hilo.”
Habari hizo zilisambaa na kukusanya
kundi la watu kutoka mji wa Mbalizi na kusababisha polisi kutumia mabomu ya
machozi kuwatawanya.
Alisema baadaye polisi walikwenda
nyumbani kwa mwanamke huyo na kumkamata, pia waliupeleka mwili wa Baraka,
Hospitali Teule ya Ifisi kwa ajili ya kuuhifadhi.
Kamanda Kidavashari alisema
mtuhumiwa alipelekwa Kituo cha Polisi Mbalizi kuhojiwa.
Umati wa watu pia ulijazana Mtaa wa
Shigamba na kusababisha polisi walipue mabomu ya machozi ili kuwatawanya
watu.
Jitihada hizo zilizaa matunda kwa
muda mfupi, lakini ilipofika saa 8:00 mchana watu wasiofahamika waliichoma moto
nyumba ya mwanamke huyo.
Katika kukabiliana na tukio hilo,
polisi waliwatawanya wananchi kwa kupiga baadhi ya watu waliokutwa eneo la
tukio. Kamanda Kidavashari alisema polisi wanawasaka watu waliohusika kuchoma
moto nyumba ya mwanamke huyo.
Mwanamke Aishia Mikononi mwa Polisi Baada Ya Kukutwa Akifukua Maiti ya Mwanaye........Aliamini Atafufuka Baada ya Siku 3
Reviewed by KUSAGANEWS
on
February 19, 2017
Rating:
No comments:
Post a Comment