Mbowe Asakwa na Polisi Kila Kona.....Apewa Masaa 48 Ajisalimishe Mwenyewe Kwa Sirro. Masogange, Chid Benz Mahakamani Kesho
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, Simon Siro amesema endapo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
hataripoti kituoni kesho (saa 48 tangu jana), atatafutwa kwa namna ambayo jeshi
hilo litaona inafaa.
Mbowe ni miongoni mwa watu mashuhuri
waliotajwa hivi karibuni katika orodha ya watu 65 ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda wanaodaiwa kujua taarifa za wanaojihusisha na dawa za
kulevya.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Kamishna Siro alisema Mbowe kupitia kwa baadhi ya viongozi aliwajulisha
angeripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, Jumatano ya Februari 15,
lakini alikuwa hajaripoti hadi jana
“Jumatatu asiporipoti kutakuwa
hakuna namna ya kulizuia tena Jeshi la Polisi kutafuta namna ya kumuhoji,” alisema.
“Mheshimiwa Mbowe tunamheshimu sana
kama kiongozi wa chama kikubwa cha siasa na hata akiwa bungeni ameonekana
akipinga kwa nguvu suala la dawa za kulevya na anasikitika kuona vijana wa
Kitanzania wanateketea.
"Asitafute namna nyingine,
tunamuhitaji kwa ajili ya kumuhoji kutokana na hizi tuhuma za dawa za kulevya,” alisema Siro.
Alisema kiongozi kama Mbowe hatakiwi
kuwa mtu wa kuta- futwa. ”Jeshi la Polisi lisingependa kuwa na mvutano na
yeye, najua anajua kuwa tunamtafuta.
"Jana (juzi) tumejitahidi
kumtafuta kwa simu hajapatikana, tumekwenda nyumbani kwake hatujampata na hata
tulipokwenda mahali ambapo inasemekana anaishi sasa hatukumpata,” alisema.
Kamanda Siro alisema hafahamu ni
kwanini Mbowe haja- ripoti wakati yeye mwenyewe anapinga biashara ya dawa za
kulevya, hivyo baada ya taarifa yake ya jana, anamuomba ajitahidi aende
waonane, tofauti na hapo ni lazima atakamatwa na kuhojiwa kwa kuwa ndiyo wajibu
wa jeshi hilo.
Hata hivyo, Februari 10 akiwa
mjini Dodoma, Mbowe alise- ma hatafika polisi kwa kuitwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Paul Makonda lakini yupo tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vya
dola endapo utaratibu wa kisheria utafuatwa.
Wengine kortini
Katika hatua nyingine, Kamishna Siro
alisema operesheni ya dawa za kulevya inaendelea vizuri na kesho watuhumiwa
Agnes Gerald ‘Masogange’, Rashid Said ‘Chid Mapenzi’ na Walid Nasher
watapelekwa mahakamani.
Hata hivyo, Kamanda Siro alitoa
kauli mbili zinazokinzana, mwanzo alisema watuhumiwa hao watashtakiwa kwa
kutumia dawa za kulevya, lakini baadaye akasema walipatikana na dawa
hizo.
Alisema operesheni inayoendelea
tangu Februari 16 imewezesha kukamatwa watuhumiwa 73 wa makosa mbalimbali, yakiwamo
ya wizi wa kutumia nguvu.
Pia, ilikamatwa mitambo mitano ya
kutengeneza pombe haramu aina ya gongo na puli 250 za bangi. Kamishna Siro
alisema juzi walimkamata mtuhumiwa anayejifanya askari magereza akiwa na sare
za jeshi hilo.
Alisema mtuhumiwa huyo, Elias
Msingwa aliwahi kuwa askari wa jeshi hilo kabla ya kuachishwa kazi Desemba
mwaka jana, akiwa na cheo cha Koplo lakini amekamatwa akiwa na sare zikiwa na
cheo cha Sajenti.
Akizungumzia tukio hilo katika Kituo
Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, akiwa na pingu mkononi, Msingwa alisema alikuwa
askari katika Gereza la Keko jijini Dar es Salaam na alifanya kitendo hicho
baada ya kukosa nauli ya daladala.
“Ninakaa Kivule jana (juzi) nilikuwa
sina nauli ya kuja mjini ndiyo maana nikavaa sare hizi ili niweze kusafiri
bure, ninaomba radhi kwa Watanzania na kuwashauri wenzangu wasije wakafanya
hivi na baada ya hapa nitazirudisha sare hizi,” alisema Msingwa.
Kamishna Siro alisema sare hizo
zilivaliwa kinyume na sheria, huku zikitumika kuwababaisha wananchi hivyo
upelelezi unaendelea utakapokamilika jalada lake litapelekwa kwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.
Mbowe Asakwa na Polisi Kila Kona.....Apewa Masaa 48 Ajisalimishe Mwenyewe Kwa Sirro. Masogange, Chid Benz Mahakamani Kesho
Reviewed by KUSAGANEWS
on
February 19, 2017
Rating:
No comments:
Post a Comment