Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema
hadi kufikia Oktoba mwaka huu, Serikali imekwishapeleka zaidi ya sh. bilioni
177 kwenye halmashauri mbalimbali nchini ili kutekeleza miradi ya maendeleo.
Ametoa kauli hiyo jana
(Alhamisi, Novemba 3, 2016) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali
lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Bibi Munde Tambwe aliyetaka kupata
kauli ya Serikali kuhusu ucheleweshwaji wa fedha za bajeti ya maendeleo katika
halmashauri mbalimbali nchini.
“Kwa kuwa Serikali ina mifumo,
miongozo, sheria na taratibu za kupeleka fedha kwenye halmashauri mara baada ya
kikao cha bajeti. Mheshimiwa Waziri Mkuu unatoa kauli gani kuhusu
ucheleweshwaji wa fedha hizo katika halmashauri nchini zikiwemo za mkoa wa
Tabora? Alihoji Mheshimiwa Munde.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu
alisema: “Baada ya Bunge kuridhia na kutoa mamlaka ya matumizi ya fedha,
Serikali ilianza kujiridhisha uwepo wa mfumo sahihi ya makusanyo na mapato na
matumizi yake. Ni kweli kwamba Serikali yetu baada ya kikao cha bajeti
inawajibika kutekeleza maamuzi ya Bunge kwa kupeleka fedha zilizopangwa.”
Waziri Mkuu alisema Serikali ilianza
kupeleka watumishi watakaosimamia ukusanyaji mapato katika halmashauri zote
nchini. Kutathmini miradi yote iliyoanza ambayo haijaendelezwa pamoja na mipya
ili kutambua thamani na kisha kupeleka fedha.
Alisema Serikali itaendelea na
upelekaji wa fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za
maendeleo. Alizisisitiza halmashauri hizo kuendelea kukusanya mapato ndani ili
kuongezea bajeti kwa fedha wanazopelekewa na watumie mfumo wa kielektroniki ili
kudhibiti mapato hayo.
Aidha, Waziri Mkuu alizitaka
halmashauri zote nchini zihakikishe fedha zinazopelekwa katika maeneo yao
zinatumika kama ilivyokusudiwa kwa miradi husuka. Aliwasihi Wabunge wafuatilie
na wasimamie matumizi ya fedha hizo ili miradi iliyopangwa iweze kukamilika.
Wakati huo huo; Waziri Mkuu alisema Serikali haijafilisika na kuhusu suala
la mfuko wa jimbo bado unatambulika na fedha zitapelekwa kwenye majimbo na
wabunge watajulishwa kiasi kilichopelekwa ili waweze kuratibu miradi yao ya
maendeleo.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati
akijibu swali la mbunge wa jimbo la Ukonga Mheshimiwa Mwita Waitara aliyetaka
kupatiwa kauli ya Serikali kuhusu kutopelekwa kwa fedha za mfuko wa jimbo.
Pia Mheshimiwa Waitara alilalamikia
kitendo cha jimbo lake kutengewa fedha kidogo katika mgawo wa mfuko wa jimbo
ambazo ni sh. milioni 16 licha ya kuwa na wananchi wengi huku jimbo la Segerea
alilosemma lina watu wachache likitengewa sh. milioni 33. Aliiomba Serikali
ingalie upya ugawaji huo kulingana na mazingira ya jimbo husika.
Waziri Mkuu alisema kumejitokeza
matatizo kwenye halmashauri zenye majimbo zaidi ya moja na Serikali inaendelea
kufanya sensa kutambua idadi ya wananchi kwenye majimbo hayo ili itakapopeleka
fedha iweze kuzingatia idadi hiyo na kuwawezesha wabunge kupanga miradi ya
maendeleo.
Waziri Mkuu: Serikali Haijafilisika
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 04, 2016
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 04, 2016
Rating:


No comments:
Post a Comment