Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA)
- imeendelea kuwataka Wakulima kufuatilia kwa ukaribu Taarifa za hali ya hewa
pamoja na kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa kilimo.
Hatua hiyo inatokana na uwepo wa
dalili za upungufu wa mvua katika mwezi Novemba kwenye maeneo mengi nchini
jambo ambalo linaweza kuathiri uzalishaji katika kilimo.
Hayo yamebainishwa jana Jijini Dar
es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini Dkt. Agnes
Kijazi alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari ambapo alisema hadi sasa
bado kuna viashiria vingi vya upungufu wa mvua ikiwa ni pamoja na kupungua kwa
Joto katika eneo la kati la Bahari ya Pasifiki kitendo ambacho kinafahamika
kama LANINA.
Alibainisha kuwa hali hiyo
inapojitokeza husababisha ukame hivyo kwa wakulima kuzingatia maelekezo ya
wataalam wa kilimo kwa kulima mazao ya muda mfupi na yanayostahamili ukame.
Dkt. Kijazi aliongeza kuwa Mamlaka
hiyo imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu mienendo ya ya unyevunyevu katika maeneo
mbalimbali nchini pamoja na Joto katika Bahari ya Hindi ambapo imebainika kuwa
hali ya unyevunyevu inaendelea kupungua katika maeneo mbalimbali nchini huku
Joto katika Bahari ya Hindi ikionekana kuendelea kupungua mambo ambayo ni
dalili za upungufu wa mvua na ukame.
Aidha Dkt. Kijazi alizungumzia
tatizo la kutokea kwa mvua za mawe katika baadhi ya maeneo nchini ambapo
alibainisha kuwa tatizo hilo linasababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa
ambayo hupelekea kutokea kwa aina ya mawingu inayofahamika kama mawingu ng’amba
hivyo suala hilo halina sababu za kuhusianishwa na Imani za kishirikina kama
ambavyo baadhi ya watu wamekua wakidhania.
TMA yatahadharisha nchi kukumbwa na ukame
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 04, 2016
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 04, 2016
Rating:


No comments:
Post a Comment