MBUNGE wa Mwibara, Kangi Lugora
(CCM) amewaonya baadhi ya mawaziri kutompotosha Rais John Magufuli kuwa fedha
zimepotea, kutokana na baadhi ya watu kuficha majumbani kwenye magodoro wakati
hiyo si sababu.
Sambamba na hilo, amewaonya wabunge
wa upinzani, kuacha kuwatumia vibaya wananchi na kuwachonganisha na Rais wao,
baada ya kuona wamebanwa kulipa kodi.
Mbunge huyo alitoa onyo hilo jana
wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka
2017/2018 na Mwongozo wa kuandaa mpango wa bajeti ya serikali kwa mwaka
2017/2018 uliowasilishwa juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.
“Nyinyi mawaziri ni abiria na mmekaa
siti za mbele kwenye gari analoendesha Rais Magufuli msimkimbize, baadhi yenu
msimpotoshe rais yeye si mchumi mtamletea matatizo mbeleni, pesa zimepotea si
kwa sababu zimefichwa kwenye magodoro ila zimepotea kwa sababu pesa zote
zimewekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zitoeni pesa hizo ziende kwenye
mabenki,” alisema.
Alisema Bunge limepoteza mwelekeo,
limekuwa la kulialia na kumlaumu Rais Magufuli kwa sababu amebana wakwepa kodi
na kufafanua “Rais aliliomba Bunge hili limsaidie kutumbua majibu, tumsaidie
mipango ya serikali iweze kutekelezeka ili kujenga nchi yetu, najua Rais ana
nia njema na nchi, Hapa Kazi Tu inawafanya wafanyabiashara waliozoea kukwepa
kodi wamebanwa sasa wanalia biashara imekufa, watumishi waliozoea posho za hapa
na pale, kusafiri wamebanwa, wabunge tuliozoea kula andazi la inchi 18 sasa
tunakula la sentimita mbili, kwenye kamati tumebanwa posho, tunalialia kisa tumeshikwa
pabaya na kuwaingiza wananchi wanyonge eti hawana pesa.
"Kiongozi wa Upinzani, Freeman
Mbowe umepewa gari na serikali na mafuta unawekewa, yamejaa kwenye gari,
kiyoyozi kipo saa 24 unasema serikali imefilisika huku unawachonganisha
wananchi na Rais wao, unawatumia vibaya wananchi, Msigwa kama Mchungaji (Peter,
Mbunge wa Iringa Mjini) tumia taaluma yako kuwashauri wenzako wawe kwenye
safari hii... Rais Magufuli anatupeleka Kaanani kuishi maisha mazuri,
ametupandisha basi kutupeleka nchi ya ahadi.
"Nashauri anapoendesha gari
ajue kuna matuta, akiendesha vibaya Watanzania atatuangusha, kuna zebra na
wanafunzi wanavuka, akiona spidi iko 50 apunguze mwendo... na nyinyi mawaziri
mmekaa siti za mbele za gari la Rais, msimpotoshe”, alifafanua.
Mbunge wa Mtera, Livingstone
Lusinde(CCM) alisema ni lazima uchumi unapokua, uoneshe kwenye maisha ya
wananchi wa vijijini ; na si kuonesha ujuaji wa pointi kwenye makaratasi.
Alisema “Upinzani msizunguke
kusema serikali imefilisika, semeni ukweli, Mbowe umefilisika, umeshindwa
kulipa madeni, serikali haijafilisika, inalipa mishahara, inalipa madeni yake”.
Naye Mbunge wa Bunda Mjini, Esther
Bulaya (Chadema) alisema kila sehemu kuna njaa, mtaani wananchi wanalia hakuna
pesa na hata wabunge wamepauka kwa kukosa fedha.
Lugora: Mawaziri acheni kumpotosha Rais
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 04, 2016
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 04, 2016
Rating:


No comments:
Post a Comment