Wakati askari polisi saba watatoa
ushahidi mahakamani katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Arusha
Mjini (Chadema), Godbless Lema, Mahakama imetoa onyo kwa askari Polisi na
Magereza wanaowasumbua waandishi wa habari na wananchi.
Onyo hilo lilitolewa na Hakimu Mkazi
Mfa- widhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Augustino Rwezile baada ya askari
Magereza kuwafukuza kwa mbio huku wakiwa na silaha waandishi wa habari
waliotaka kuchukua kumbukumbu za Lema kufikishwa mahakamani.
Pia, aliwaonya Polisi ambao wamekuwa
wakilalamikiwa kwa kuwazuia wananchi wanapokwenda kusikiliza kesi ya mbunge
wao.
Waandishi wa habari jana waliwahi
asubuhi kusikiliza kesi ya Lema na kutaka kumpiga picha wakati akifikishwa mahakamani,
lakini walipata wakati mgumu baada ya kukimbizwa na askari Magereza wenye
silaha ambao hawakutaka mtu yeyote kupiga picha ya mtuhumiwa huyo.
Waandishi hao, Lilian Joel (Uhuru)
na Janet Mushi (Mtanzania) waliokolewa na Hakimu Mkazi, Nestory Baro ambaye
walimshika huku wakipiga kelele kuomba msaada hatua ambayo ilizua tafrani
mahakamani.
Hata hivyo, baada ya tukio hilo,
waandishi hao walipelekwa na hakimu Baro kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Rwezile
ambaye alishuhudia pia tukio hilo.
Hakimu Rwezile aliwaita maofisa wa
Polisi, waliokuwa mahakamani hapo na kuwaonya kuacha tabia ya kuwakamata na
kuwabughudhi wananchi na wanahabari wanaofika mahakamani hapo kusikiliza kesi.
Hakimu Rwezile, pia alilitoa agizo
hilo la kuwaonya askari Magereza na Polisi baada ya wakili wa Lema, John Mallya
kuomba tamko la mahakama kutokana na wananchi kuzuiwa kuingia mahakamani,
kukamatwa na kunyanyaswa waandishi wa habari.
Hakimu Rwezile alitoa agizo tena kwa
askari Magereza na Polisi wanaofika mahakamani kuacha kuwasumbua wananchi na
kueleza pamoja na wanahabari wana uhuru wa kufika mahakamani na kusikiliza
kesi.
“Hakuna usiri mahakamani hatutarajii
tena kuona misuguano hapa, tayari nimezungumza na waandishi na askari Magereza
kuhusiana na suala hili, eneo hili lipo chini ya Mahakama hivyo watu wanapaswa
kuingia na kutoka salama,” alisema
Jana saa mbili asubuhi, Lema
alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kwa basi la Magereza, akiwa
chini ya ulinzi mkali na haikuruhusiwa kumpiga picha.
Mbele ya Hakimu Rwezile, wakili wa
Serikali, Fortunatus Mhalila alisoma maelezo ya awali ya kesi hiyo na kudai
upelelezi umekamilika na upande wa Jamhuri una mashahidi saba.
Aliwataja mashahidi hao kuwa ni
Ofisa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Arusha (RCO), SSP George Katabazi, Mkuu wa
Upelelezi wa Polisi Wilaya ya Arusha (OSCID), ASP Damas Masawe, Mkaguzi wa
Polisi, Adam Nyamiti, WP 6826 Ester Yohana na Ofisa wa Kitengo cha Upelelezi
Makosa ya Mtandao Makao Makuu ya Polisi, Ezekiel Kway.
Alidai katika kesi hiyo, Lema
anatuhumiwa kuhamamisisha watu kutenda kosa ikiwa ni kinyume na kifungu 390
(35) cha Kanuni za Adhabu, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mhalila alidai Lema kati ya Agosti
Mosi hadi 26, alitengeneza na kusambaza ujumbe mfupi wa sauti kupitia WhatsApp
kuhamasisha watu kutenda kosa, ikiwapo kuwataka kufanya maandamano kuanzia
Septemba Mosi mwaka huu. Baada ya maelezo hayo, Hakimu Rwezile alimtaka Lema
kueleza kama maelezo hayo ni sahihi au la.
Lema alikanusha kutuma ujumbe wa
kuhamamisha uvunjaji wa sheria. Wakili Mallya alisema upande wa utetezi upo
tayari kupangwa kwa siku ya kuanza kuwasikiliza mashahidi. Kutokana na maelezo
hao, Hakimu Rwezile aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 2, ushahidi utakapoanza
kutolewa.
Lema na mkewe, pia wana kesi
nyingine ya kutoa lugha ya uchochezi dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho
Gambo ambayo nayo iliahirishwa hadi Desemba 21 kutokana na mtuhumiwa wa pili,
Neema Lema (33) kutokuwapo mahakamani.
Wakili Mallya alisema Neema ameitwa
jijini Dar es Salaam katika kesi nyingine. Baada ya maelezo hayo, Hakimu
Rwezile aliahirisha kesi hiyo na Lema kurejeshwa magereza hadi leo, Mahakama
Kuu Kanda ya Arusha itakapoanza kusikiliza maombi ya dhamana.
Wanahabari Watimuliwa kwa Bunduki Kesi ya Lema....Mahakama Yatoa Onyo Kali kwa Jeshi la Polisi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 17, 2016
Rating:
No comments:
Post a Comment