Hatimaye Mahakama Kuu Kitengo cha
Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Ufisadi imeanza
rasmi usikilizaji wa kesi jana.
Kesi ya kwanza kutua na kusikilizwa
na Mahakama hiyo ambayo inatokana na ahadi za Rais John Magufuli aliyoitoa
wakati wa kampeni zake ni ya uhujumu uchumi inayowakabili Mtanzania mmoja na
raia wa China na mwingine wa India.
Kwa pamoja washtakiwa hao
wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wakidaiwa kukutwa na nyavu haramu za kuvulia
samaki zilizopigwa marufuku zenye thamani ya zaidi ya Sh7.4 bilioni.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi
ya msingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini wamefungua maombi ya
dhamana katika Mahakama hiyo na hivyo kuweka rekodi ya kuwa kesi ya kwanza
kusikilizwa.
Hata hivyo, maombi hayo yamewekewa
pingamizi na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akipinga washtakiwa hao
kupewa dhamana akidai yamefunguliwa kwenye Mahakama isiyo sahihi.
Pingamizi hilo lilisikilizwa jana na
Jaji Rehema Mkuye na baada ya hoja za pande zote alipanga kutoa uamuzi Novemba
14.
Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi
hilo mvutano mkali wa kisheria uliibuka baina ya upande wa mashtaka na utetezi
kuhusu tafsiri ya Mahakama Kuu.
Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Timon
Vitalis alidai kuwa sheria inatamka kuwa Mahakama Kuu na siyo Mahakama ya
Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Wakili huyo alidai Mahakama hiyo (ya
ufisadi) inakuwa na uwezo wa kutoa dhamana pale kesi ya msingi inakuwa tayari
imeshafunguliwa mahakamani hapo.
Hata hivyo, wakili wa washtakiwa
hao, Roman Lamwai alipinga hoja hizo akidai Mahakama hiyo ni mahali sahihi kwa
mujibu wa tafsiri ya Sheria ya Uhujumu Uchumi kama ilivyofanyiwa marekebisho.
Alisisitiza kuwa hata ukubwa wa
gharama zinazohusika katika kesi ni lazima maombi hayo yafunguliwe kwenye
Mahakama hiyo yenye jukumu la kusikiliza na kuamua kesi za rushwa na uhujumu
uchumi.
Moja ya vigezo vya kesi
zinazofunguliwa katika Mahakama hiyo ni kiwango cha fedha za rushwa au uhujumu
uchumi kinachohusika ambacho ni kuanzia Sh1 bilioni.
Hata hivyo, DPP anaweza kufungua
kesi mahakamani hapo chini ya kiwango hicho kulingana na mazingira maalumu
kadri atakavyoona kuwa inafaa.
Katika kesi ya msingi inayosikilizwa
na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Godfrey Mwambapa kwenye shitaka la
kwanza washtakiwa Feng na Kerenge wanadaiwa kutenda kosa la uhujumu uchumi kwa
kuagiza nyavu haramu nje ya nchi.
Kesi ya kwanza yaanza Kusikilizwa Mahakama ya Mafisadi Dar
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 04, 2016
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 04, 2016
Rating:


No comments:
Post a Comment