Mtoto mdogo mwenye umri wa
miaka mitatu mkazi wa Kijiji cha Nyamihaga Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma
amekufa baada ya kunajisiwa na baba yake wa kambo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma,
Ferdinand Mtui alisema jana kwamba wamemtia mbaroni mtuhumiwa Hamimu Saidi (27)
mkazi wa kijiji hicho cha Nyamihaga.
Akitoa maelekezo kuhusu mkasa huo,
Kamanda Mtui alisema mtuhumiwa alitekeleza dhamira yake hiyo wakati mama wa
mtoto huyo ambaye alikuwa mke wa mtuhumiwa alipokwenda kisimani kuchota maji.
Alisema baada ya mwanamke huyo
kurejea nyumbani kutoka kisimani alimshuhudia mtoto wake akilalamika sana
wakati akitaka kujisaidia haja ndogo na ndipo alipomchunguza akagundua kwamba
mtoto huyo alikuwa ameingiliwa na kujeruhiwa kwenye sehemu zake za siri.
Kamanda Mtui alisema baada ya
kugundua hilo, mama huyo wa mtoto alimchukua mtoto huyo na kumpeleka Hospitali
ya Mkoa ya Maweni kwa matibabu, ambako iligunduliwa kuwa mtoto huyo alikuwa
amenajisiwa na alikuwa amebanwa shingo wakati akifanyiwa kitendo hicho hivyo
alikosa pumzi wakati akifanyiwa unyama huo.
Kamanda huyo alisema hata hivyo
mtoto huyo alifariki katika Hospitali ya Mkoa ya Maweni alipokuwa akitibiwa na
kwamba baada ya uchunguzi wa kidaktari na uchunguzi wa Polisi, mwili wa mtoto
huyo ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.
“Kwa sasa mtuhumiwa Hamimu Saidi
anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Kigoma wakati upelelezi
ukiendelea ili taratibu za kumfikisha mahakamani zifanyike na kwamba anatarajia
kufikishwa mahakamani wakati wowote upelelezi huo utakapokamilika,” alieleza Kamanda Mtui.
Baba Wa Kambo Atiwa Mbaroni kwa Kumnajisi Hadi Kufa Mtoto wa Miaka Mitatu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 21, 2016
Rating:
No comments:
Post a Comment