Jaribio jingine la maombi ya dhamana
ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema linafanyika leo baada ya
kusota mahabusu tangu akamatwe mkoani Dodoma Novemba 3.
Lema anayekabiliwa na tuhuma ya
kutoa lugha ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli, ombi hilo la dhamana
linakuwa la tatu baada ya kukwama mara mbili tangu alipoingizwa mahabusu.
Lema ambaye anatetewa na mawakili
sita; Peter Kibatala, John Mallya, Charles Adiel, Adam Jabir, Faraja Mangula na
Sheck Mfinanga, dhamana yake licha ya kutolewa na Hakimu Mkazi, Desdery
Kamugisha ilipingwa kutokana na notisi ya rufani iliyowasilishwa na mawakili wa
Serikali.
Baada ya notisi hiyo, Lema aliandika
barua Mahakama Kuu kuomba mapitio ya kesi hiyo kwa maelezo kuwa taratibu za
kisheria zilikiukwa kutokana na hakimu kutoa dhamana lakini akashindwa
kukamilisha masharti ya dhamana na kupokea hoja za Jamhuri.
Hata hivyo, wakili mwandamizi wa
Serikali, Paul Kadushi aliwasilisha pingamizi jingine kupinga Mahakama Kuu
kufanya marejeo ya kesi hiyo.
Kadushi aliwasilisha hoja mbili za
kisheria juu ya kuweka pingamizi la ombi la mbunge huyo kuwa muombaji hakukidhi
vigezo vya kuiomba mahakama irejee maamuzi ya mahakama kwa kuwa badala ya
kuiandikia mahakama barua ya kuomba ifanye mapitio ya maamuzi hayo, angetakiwa
akate rufaa juu ya maamuzi ya mahakama.
Pia, alisema maombi hayo yamekinzana
na Sheria ya Mahakama za Hakimu kifungu (43) (2) kutokana na mahakama hiyo
kutokuwa na uwezo wa kupokea ombi ama kukata rufaa kwa maamuzi hayo, kwa kuwa
ni madogo.
Hata hivyo, mawakili wa Lema
walipinga hoja hizo na kueleza sheria zinaruhusu mlalamikaji kuandika barua
kuomba mapitio, na tayari suala hilo limewahi kufanyika hata kwa ofisi na
mwanasheria mkuu kuomba mapitio.
Wakili Kibatala alisema Mahakama Kuu
ina mamlaka ya kisheria yenyewe kufanya mapitio ya kesi hata kama hakuna
aliyelalamika na tayari imewahi kufanya mapitio kwa kesi kadhaa.
Baada ya hoja za pande zote kutolewa
Jaji Sekela Moshi aliomba kupewa muda, kupitia hoja zote zilizoletwa na pande
zote ili kuzifanyia maamuzi leo.
Godbless Lema Kujaribu Tena Bahati yake Leo Mahakamani baada ya Kusota Mahabusu kwa Siku 19
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 21, 2016
Rating:
No comments:
Post a Comment