MTENDAJI WA KIJIJI CHA NYAMBUNDA WILAYANI KIBITI APIGWA RISASI



MTENDAJI wa kijiji cha Nyambunda ,mkazi wa Kijiji cha Nyambunda Kata ya Bungu wilaya ya Kibiti ,mkoani Pwani,Ally Omary Milandu (58),amepigwa risasi ya kisogoni na kutokea mbele ya paji la uso na watu wasiojulikana na kufa papo hapo.

Tukio hilo ni la tatu kutokea likihusisha viongozi wa serikali za vijiji na tarafa mkoani humo ikiwemo wilaya ya Mkuranga na Kibiti.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Boniventure Mushongi akifafanua juu ya tukio hilo alisema limetokea oct 24 ,majira ya saa mbili usiku.

Alisema watu watatu wasiofahamika wakiwa kwenye pikipiki aina ya boxer waliwavamia Ally Omary Milandu ambaye ni Mtendaji wa Kijiji cha Nyambunda na Abdul Salim Msemeo (43) Mganga wa Zahanati ya Nyambunda wakiwa wamekaa kibarazani kwa mtendaji huyo wakipunga upepo .

Kamanda Mushongi alieleza waliwaamuriwa watulie walipo ndipo waliteremka watu wawili waliokuwa wamepakiwa kwenye pikipiki hiyo na kuchomoa bunduki walizokuwa wameweka mgongoni na kuwashambulia.

Alisema mtendaji wa Kijiji hicho Ally Milandu alipigwa risasi ya kisogoni iliyotokea mbele ya paji la uso wakati akijaribu kukimbia kuingia ndani ya nyumba yake ambapo alianguka na kufariki papo hapo.

Kamanda Mushongi alisema kwamba mwenzie aliyekuwa naye aliweza kunusurika baada ya kufanikiwa kukimbia na kwenda kujificha nyumba ya jirani na hapo na kutokana na kiza watu waliofanya mauaji hayo walishindwa kumuona.

Kwa mujibu wa kamanda huyo ,jeshi la polisi mkoa wa Pwani wanaendesha msako mkali wa kuwasaka waliohusika na tukio hilo.

Hata hivyo kamanda Mushongi aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano mara watakapowabaini ama kuwa na shaka na watu ambao ni wahalifu .

“Yeyote anaweza kutumia namba ya simu 0715 00 99 53 ili waliohusika waweza kupatikana na kuchukuliwa hatua stahiki.

MTENDAJI WA KIJIJI CHA NYAMBUNDA WILAYANI KIBITI APIGWA RISASI MTENDAJI WA KIJIJI CHA NYAMBUNDA WILAYANI KIBITI APIGWA RISASI Reviewed by KUSAGANEWS on October 26, 2016 Rating: 5

No comments: