Mwanafunzi wa mwaka wa tatu
wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI) cha mkoani Arusha, Allan Mbando,
ameibwaga Serikali katika kesi ya kudaiwa kusambaza ujumbe kupitia Mtandao wa
Facebook akimtaka Mwamunyange apindue nchi.
Katika mtandao huo wa kijamii,
Mbando, anadaiwa kutuma ujumbe uliosomeka kwamba: “Mwamunyange pindua nchi
haiwezekani wote wawe nje, halafu hakuna aliyepewa mamlaka ya kukalia kile
kiti.”
Kutokana na madai hayo, Jeshi la
Polisi mkoani Arusha lilimfungulia mashtaka Mbando ya kudaiwa kusambaza ujumbe
huo uliokusudia kueneza na kufanya uchochezi.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo mjini
hapa juzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha,
Augustine Rwizile, alisema mahakama hiyo imepitia kwa kina hoja na ushahidi wa
pande zote mbili katika kesi hiyo.
Hakimu Rwizile alisema baada ya
kupitia ushahidi katika kesi hiyo, mahakama imejiridhisha kuwa upande wa
Jamhuri katika kesi hiyo haukuweza kuwasilisha ushahidi unaoweza kumtia hatiani
mshtakiwa.
Alisema mbali na ushahidi huo
kutojitosheleza, pia hapakuwapo na jambo lolote lenye nia ovu ya kusababisha au
kufanya uchochezi katika ujumbe uliosambazwa na mshtakiwa.
“Sasa mahakama hii inamwachia huru
mshtakiwa baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka yake
pasipo kuacha shaka yoyote.
“Lakini pia kama kutakuwa na upande
ambao haujaridhika katika hukumu hii unaweza kukata rufaa,” alisema Rwizile.
Akisoma hukumu hiyo, alisema ujumbe
uliosambazwa haukuwa na umuhimu wowote kwa kuwa haukumwelezea Mwamunyange ni
nani katika nchi anayotakiwa kuipindua huku pia ujumbe huo ukiwa haukutaja nchi
iliyolengwa kupinduliwa.
“Ujumbe ulioandikwa katika Facebook
haumtambulishi Mwamunyange ni nani. Lakini ujumbe hauonyeshi jambo la msingi lenye
uhusiano wa kisiasa katika Taifa linalodaiwa,” alisema Rwizile.
Kutokana na sababu hizo ikiwamo
ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo kushindwa kuthibitisha ujumbe
uliosambazwa na mshtakiwa, mahakama ililazimika kumwachia mshtakiwa.
Mshtakiwa huyo katika kesi hiyo
alikuwa akitetewa na Wakili Moses Mahuna.
Mbando anaongeza idadi ya watu
walioshtakiwa mahakamani kutokana na makosa ya mtandaoni baada ya Aprili, mwaka
huu mkazi mwingine wa Arusha, Isack Habakuki (40), kufikishwa mahakamani na
kusomewa mashtaka ya kusambaza lugha ya matusi na dhihaka kwa Rais Dk. John
Magufuli.
Baada ya kesi hiyo kuendelea kusomwa
mahakamani hapo, Isack alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa
faini ya Sh milioni saba na yeye alikubali kuzilipa kwa awamu.
Mtu mwingine aliyeshtakiwa Aprili,
mwaka huu kwa makosa ya mtandaoni ni kondakta wa daladala, Hamimu Seif (42),
aliyepandishwa kizimbani kwa kosa analodaiwa kulifanya Machi 10, mwaka huu
alipotishia kumuua Rais Magufuli kwa maneno akiwa katika Baa ya Soweto iliyopo
Makumbusho, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Aliyetaka Mwamunyage apindue nchi ashinda kesi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
October 09, 2016
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
October 09, 2016
Rating:


No comments:
Post a Comment