Sheikh Abubakar Zuberi, ameteuliwa na chombo hicho muhimu ndani ya Bakwata kuwa Kaimu Mufti wa Tanzania baada ya kupata kura zote nane za wajumbe wa Baraza hilo, waliokutana leo Juni 22, 2015 jijini Dar es Salaam.
Kabla ya uteuzi huo, Sheikh Abubakar Zuberi alikuwa Naibu Mufiti wa Sheikh Mkuu wa Tanzania na pia Mjumbe wa Baraza Kuu hilo la Ulamaa nchini.
Taarifa zilizoifikia Gumzo Tz Na Fikra Pevu zinasema kuwa Sheikh Zuberi, amechukua nafasi hiyo, kufuatia kifo cha aliyekuwa Mufti wa Tanzania, Issa Shaaban bin Simba, huku ikielezwa kwamba katika siku 90 hizo za mpito za uongozi wa chombo hicho kikuu cha Waislamu nchini, atasimamia pamoja na mambo mengine Uchaguzi Mkuu wa Mufiti mwingine.
Baraza la Masheikh la Ulamaa linaundwa na wasomi waliobobea kwenye masuala ya dini. Hilo ndilo lenye mamlaka ya kumchagua mtu wa kushika nafasi hiyo kwa muda. Miongoni mwa wajumbe wake, yumo pia Kadhi Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abddalah Mnyasi.
Wajumbe wengine ni Sheikh Ally Mukoyagile, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Salum Mfereji, Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya, Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Kiburwa na Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Hamid Masoud Jongo.
Katika mtandao maarufu wa kijamii nchini wa JamiiForums, kumekuwepo na mjadala mzito juu ya uteuzi huo. Baadhi ya wanachama wa mtandao huo, walikuwa wakiwataja Kadhi Mkuu, Sheikh Mnyasi na Sheikh Mkoyogile kama watu sahihi wa kumrithi Marehemu Mufiti, Sheikh Issa Shabaan bin Simba.