LISHE duni miongoni mwa watoto na vijana walioko katika ngazi mbalimbali za elimu, imetajwa kuwa moja ya sababu zinazochangia kudumaa na kuzorota kwa kiwango cha elimu nchini.
Kwa mujibu wa wataalam wa afya na lishe, tatizo hilo la lishe duni kwa vijana wa Taifa hili walioko mashuleni, huweza kuwasababishia udumavu wa ubongo na akili, huku ikielezwa kwamba asilimia 42 ya watoto na vijana wa rika hilo, wanakabiliwa na tatizo hilo, hali inayoathiri uwezo wao wa kufundishika wanapokuwa darasani, hivyo ufaulu wao wa mitihani kuwa duni pia.
Dk. Joyceline Kaganda ni Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe nchini. Akielezea tatizo hilo la lishe duni katika mkutano uliohusiana na masuala ya Lishe jijini Arusha mwaka huu wa 2015, anasema sababu kubwa inayowafanya watoto walioko mashuleni wapate shida kujifunza na hata kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao, ni udumavu wa akili na ubongo unaosababishwa na lishe duni.
”Taifa hili bado linakabiliwa na tatizo la uelewa mdogo wa wananchi wake juu ya mahusiano kati ya lishe na maendeleo ya mtoto kitaaluma,” FikraPevu ilimkarirri Dk Joyceline.
”Kipimo kikubwa tunachokitumia katika kupima hali ya udumavu wa ubungo na akili ya watoto wenye umri kati ya miaka 0 hadi mitano, ni lishe. Kama mtoto mwenye umri huo hakupata lishe yenye virutubisho muhimu mwilini, lazima atadumaa tu ubungo na akili.
”Lakini matatizo yote haya yanaanzia kwa kina mama tangu wanapokuwa wajawazito. Katika kipindi hicho cha ujauzito hadi kujifungua kina mama wanahitaji kupata lishe bora ili mtoto aliyeko tumboni aweze kukua vizuri kimwili, kiakili na kuwa na afya bora kwa ujumla.”
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa Lishe, watoto wanaokua wakiwa na udumavu wa akili tangu wakiwa tumboni mwa mama zao hadi kufikia umri wa utu uzima, kiwango chao cha utendaji kazi kinakuwa kidogo, na hata uwezo wao wa kufikiri unakuwa mdogo pia.
”Ndiyo maana tunawasihi kila mara kina mama wapende kujielimisha juu ya masuala ya lishe, kwani hiyo itawasaidia wao wenyewe kuwa na afya bora, lakini pia na watoto wao,” anasisitiza.
Anavitaja baadhi ya vyakula muhimu kwa lishe ya mama na mtoto kuwa ni pamoja na mboga mboga na matunda, samaki, maharagwe pamoja na vyakula vya wanga kama vile wali, ugali unaotokana na nafaka halisi za mahindi au mtama usikobolewa.
”Suala la lishe likitiliwa mkazo litasaidia sana kukua kwa elimu nchini pamoja na kuchochea maendeleo ya jamii kwa ujumla,” anasema Dk. Joyceline.
”Suala la lishe likitiliwa mkazo litasaidia sana kukua kwa elimu nchini pamoja na kuchochea maendeleo ya jamii kwa ujumla,” anasema Dk. Joyceline.
Kwa upande wake, Profesa Joyce Kinabo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro, Kitovu cha Kilimo na Lishe anasema Taifa lolote lile duniani haliwezi kupiga hatua ya maendeleo kama wananchi wake wana tatizo la lishe duni kwa maelezo kuwa maendeleo katika sekta zote, yanategemea lishe bora.
”Mtu mwenye Lishe bora anaweza kufanya shughuli za uzalishaji kwa ubora na ufanisi zaidi wa hali ya juu hivyo kujiletea maendeleo yeye na jamii yake pamoja na taifa kwa ujumla,” anasema Profesa Joyce.
Kutokana na hali hiyo Mtaalamu huyo anashauri Serikali na mashirika binafsi nchini kutilia mkazo suala zima la umuhimu wa lishe bora kwa ajili ya ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.
Katika hilo anahimiza kwa kusema: ”Elimu ya masuala ya lishe nchini itolewe kuanzia ngazi ya familia, mashuleni na vyuoni ili kila mwananchi awe na uelewa mkubwa juu ya masuala ya lishe, hivyo kuliondoa Taifa kwenye tatizo la kuwa na lishe duni kwa sababu Watanzania wengi hawana uelewa juu ya masuala ya lishe.
”Matatizo ya udumavu wa akili na ubongo, magonjwa ya utapiamlo na kwashakoo, bado ni makubwa hivyo elimu zaidi juu ya lishe inahitajika.
“Miaka ya nyuma, elimu juu ya masuala ya lishe ilikuwa inatolewa mashuleni, lakini baadaye ilisitishwa… sijui umuhimu wa somo hilo haukuonekana, lakini sasa ni wakati muafaka wa kulirudisha somo hili mashuleni.”
Kwa mujibu wa Profesa huyo wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, upo ulazima mkubwa kwa Serikali na watunga sera kutambua uhusiano uliopo baina ya lishe bora kwa watoto na jamii nzima ya Taifa hili na maendeleo ya Taifa. Kutokana na uhusiano huo, Profesa Joyce anatoa wito kwa Serikali na watunga sera, kulipa umuhimu suala zima la elimu ya lishe na virutubisho ili kuhakikisha kuwa elimu hiyo inatolewa kuanzia ngazi ya familia, mashuleni na vyuoani, kwa kuanzisha somo maaalum la lishe ili kuchochea ustawi bora wa jamii na Taifa.
”Jamii ya wafugaji, hususan Waamasai wanakabiliwa na tatizo la udumavu wa akili na ubongo, pamoja na ukondefu na upungufu wa damu mwilini kwa sababu ya kutotumia mboga na matunda katika milo yao, kwa kuwa jamii hiyo hupendelea kula nyama tu na maziwa,” anabainisha Profesa Joyce na kuongeza:
“Ndiyo maana, katika jamii hiyo ya Waamasai, unakuta asilimia 16 ya wananchi wote, wana kimo kisicholingana na umri wao…yote hii husababishwa na lishe duni.”
Profesa Tola Atinmo kutoka Chuo Kikuu cha Ibadan cha Nigeria, Kitengo cha Lishe na Virutubisho vya binadamu, katika mkutano huo wa Arusha, alielezea haki ya kupata lishe na virutubisho, akisema ni haki ya msingi ya kila binadamu kama ilivyoainishwa kwenye Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu wa mwaka 1948.
Mdau mwingine wa masuala ya Lishe, George Kajubi, kupitia mkutano huo, aliishauri Serikali kutilia mkazo suala la lishe, huku akisisitiza umuhimu wa kuongezwa kwa bajeti ya sekta lishe nchini ili kuwa na Taifa lenye watu wenye afya bora na hivyo Taifa bora pia.
”Lishe bora ni kichocheo cha ustawi bora wa maendeleo ya kiuchumi na kuwa na Taifa bora pia, hivyo zinahitajika juhudi za makusudi za kuinua kiwango cha lishe kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa.
Lishe Duni Chanzo Kikuu cha Udumavu wa Akili na Elimu kwa Watoto
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 23, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment