Takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa kila siku wanawake 24 wanafariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi ambapo kwa mwaka mmoja zaidi ya wanawake 8,600 wanakufa jambo ambalo linakwamisha malengo ya millennia.
Kaimu Mkurugenzi wa Afya ya Uzazi na Mtoto katika wizara hiyo, Dk Georgina Msemo, amezitaja sababu zinazochangia vifo hivyo kuwa ni pamoja na kina mama wajawazito kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, kuchelewa kuanza kliniki pamoja na kujifungilia katika vituo vya afya ambavyo havina huduma za kutosha za uzazi.
Kwa mujibu wa Dk Msemo, nchi ya Sirilanka ni miongoni mwa nchi duniani ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vinavyotokana na matatizo ya uzazi. Inaelezwa kwamba nchi hiyo imefanikiwa kutokana na Rais wa nchi hiyo kuhusika kwa asilimia 100 katika kampeni ya kutokomeza vifo hivyo.
Takwimu za vifo vya wajawazito na watoto nchini Tanzania vinatishia ustawi wa Taifa kutokana na  kuwepo takwimu za kutisha zinazoonyesha kuwa kwa mwaka mmoja pekee, wanawake zaidi ya 8,600 wanafariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi, huku takriban watoto 50,000 wakifariki dunia kila mwaka.
Mpango wa Serikali wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kuanzia mwaka 2008 hadi 2015 ujulikanao kama ‘One Plan’ ulipanga kuweka vifaa vya kufanyia upasuaji wa dharura kwenye vituo vingi vya afya nchini, jambo ambalo limeshindikana hadi sasa.
Hata hivyo, taarifa ya hivi karibuni ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imekuja na habari njema inayoelezea kushuka kwa idadi ya vifo vya kina mama vinavyotokana na uzazi (MMR), kutoka 578 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2005 hadi vifo 454 mwaka 2010, hivyo kufikia lengo la nne la millennia.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika kipindi kama hicho, vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 68 katika kila vizazi 1,000 hadi kufikia 54. Mwaka 2010, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 260 duniani zilizotoa ahadi kadhaa mbele ya jumuiya ya Umoja wa Mataifa (UN), za kuboresha huduma ya afya kupitia mpango wa kuboresha afya ya mama na mtoto ujulikanao kama “Kila mwanamke, kila motto.”
Katika ahadi yake hiyo, Tanzania ilipanga kuongeza bajeti ya sekta ya afya kutoka asilimia 12 hadi 15, kuongeza udahili wa wanafunzi kwenye vyuo vya afya kutoka 5,000 hadi 10,000 na kuongeza idadi ya wahitimu kwenye vyuo hivyo kutoka 3,000 mwaka huo hadi 7,000 ifikapo 2015. Lakini pia Tanzania iliahidi kuboresha upatikanaji bure wa huduma za uzazi, kuongeza huduma ya uzazi wa mpango kutoka asilimia 28 mwaka huo hadi 60 mwaka 2015, kuboresha mifumo ya mawasiliano ya simu kwenye hospitali pamoja na kuanzisha matumizi ya magari ya wagonjwa yenye gharama nafuu.
Tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 2010, nchi nyingi duniani, hasa za Kiafrika zilijitokeza na kuahidi kufanya mambo kadhaayatakayosaidia kuboresha afya ya jamii katika nchi zao. Hata hivyo, kutokana na kuendelea kuwepo kwa idadi kubwa ya vifo
vinavyotokana na uzazi nchini Tanzania, ni wazi kwamba hadi sasa Serikali imeshindwa kutimiza ahadi zake hizo za tangu mwaka 2008, za kwamba kufikia mwaka huu wa 2015, vituo vya afya vitakuwa vinatoa huduma za afya za dharura kwa asilimia 50.
Utafiti uliofanywa na GUMZO YZ  unaonyesha kuwa ni asilimia tisa tu ya vituo vya afya  nchini vinavyotoa huduma za afya za dharura, ikiwemo upasuaji. Aidha, utafiti huo umebaini kutokuwepo kwa mipango thabiti ya pamoja ya utekelezaji wa Sera ya Afya miongoni mwa wadau wakuu wa sekta hiyo kwa kuzingatia takwimu zilizopo ndani ya Serikali yenyewe.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo vya uzazi, ikielezwa kwamba hadi sasa bado tatizo la vifo vya uzazi halijapewa kipaumbele kama ambavyo mambo mengine yanapewa uzito na Serikali.
Ukubwa wa tatizo la uzazi unatazamwa kama tukio la kawaida wakati ni janga la kitaifa kwa sababu linamaliza maisha ya wanawake ambao ndiyo kiwanda cha uzalishaji wa kizazi cha Taifa la kesho. Kwa mfano, inapotokea ajali tu ya basi na kuuwa watu tuseme 20, Serikali inashituka na kuchukua hatua, lakini inapotokea wanawake 20 wakapoteza maisha kila siku kutokana na matatizo ya uzazi, Serikali hiyo hiyo inaonekana kutoshituka na kuchukua hatua madhubuti. Hapo ndipo tatizo kuu lilipo katika janga hili la Taifa.