Hali ya jiji la Dar es Salaam jana ilizidi kuwa mbaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kuwaweka wakazi kwenye hali ngumu zaidi baada ya kukumbwa na matukio mengine makubwa yaliyoathiri jiji na sehemu nyingine kote nchini tangu kuanza kwa mwaka.
Mvua hizo kubwa zinazolingana na zile zilizonyesha
miaka mitatu iliyopita na kusababisha usumbufu mkubwa, jana
zilisababisha nyumba kadhaa kuanguka, madaraja kukatika, barabara
kufungwa, ikiwapo ya Morogoro, usafiri kuwa mgumu kutokana na misururu
mirefu ya magari na Jeshi la Polisi kulazimika kutoa tamko la kushauri
wananchi kutoka mapema maofisini ili kuwahi majumbani.
Matukio hayo yametokea siku chache baada ya
kusitishwa kwa mgomo wa pili wa madereva uliosababisha usumbufu mkubwa
kwa wasafiri karibu nchi nzima. Madereva waliamua kufanya mgomo huo
kupinga masharti mapya ya kupata leseni yaliyotolewa na Serikali ikiwa
ni mkakati uliobuniwa kukabiliana na ajali ambazo tangu Januari mwaka
huu zimeua zaidi ya watu 900.
Mwaka 2015 pia umeanza kwa mgomo wa nchi nzima wa
wafanyabiashara, kuibuka upya kwa mauaji ya albino, tishio la ugaidi
lililoambatana na mauaji ya polisi na kugundulika kwa vituo vya mafunzo
ya kigaidi kwa watoto wadogo, kuporomoka kwa kasi kwa thamani ya
shilingi, kuvurugika kwa mchakato wa katiba na mvua ya mawe iliyoua watu
kadhaa mkoani Shinyanga.
Kwa muda wa siku mbili, mvua zimenyesha mfululizo
na kusababisha mafuriko kwenye sehemu kadhaa za Jiji la Dar es Salaam,
ambalo ni kitovu cha biashara na shughuli za Serikali, likiwa na
takriban watu milioni 4.4 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka
2012.
Pamoja na mvua hizo kunyesha kwa wingi jijini Dar
es Salaam, athari zake zinategemewa kugusa mikoa mingine yote kutokana
na umuhimu wa jiji kiuchumi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alisema jana kuwa daraja la Mwanamtoti lililopo eneo la
Mbagala Kuu limeng’olewa na mafuriko hayo.
Kamanda Kova alisema Barabara ya Morogoro
imefungwa eneo la kati ya Magomeni na Fire kutokana na Mto Msimbazi
kufurika na kusababisha maji kupita juu ya daraja.
Alisema nyumba za watu wanaoishi Magomeni Mikumi
zimejaa maji na hivyo Jeshi la Polisi limetoa amri kwa watu wote
kuondoka eneo hilo.
Kova alisema barabara nyingine iliyofungwa ni ya
Kinyerezi ambako maji yalikuwa yakiongezeka na kutishia kulisomba daraja
linalounganisha Kinyerezi na Majumba Sita.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Temeke, Andrew Satta
alisema daraja lililopo eneo la Mwanamtoti eneo la Mbagala Kuu
limeng’olewa na mafuriko na kusababisha kukatika kwa mawasiliano.
“Nimewaagiza vijana wangu watembelee sehemu
mbalimbali ili kuangalia maeneo ambayo yameathiriwa na mvua
zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam,” alisema Satta.
Mwaka wa shida
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 07, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment