Dar es Salaam. Hii kali, hicho ndicho unachoweza kusema wakati mashabiki wa Yanga walipoamua kuishangilia Azam ikiifunga Yanga mabao 2-1 na kuizima ndoto ya Simba kucheza mashindano ya Afrika mwakani.
Pamoja na mvua kubwa kunyesha na Uwanja kujaa maji
kiasi cha wachezaji wa timu zote mbili kushindwa kuonyesha uwezo wao,
Yanga ilipata bao la kuongoza kupitia kwa Andrey Coutinho, kabla ya Azam
kusawazisha kupitia kwa Bryson Rafael na nahodha John Bocco aliingia
akitokea benchi kupachika bao la ushindi.
Ushindi huo umeifanya Azam kufikisha pointi 48,
ambazo haziwezi kufikiwa na Simba (44), hata kama itashinda mchezo wake
wa mwisho dhidi ya JKT Ruvu. Kutokana na mvua Yanga walikabidhiwa kombe
lao ndani. Kabla mechi haijaanza mashabiki wa Yanga walimiminikia
uwanjani na kukaa jukwaa moja na wenzao wa Azam na kushangilia, huku
jukwaa ambalo hukaliwa na mashabiki wa Simba lilikuwa na mashabiki
wachache.
Saa 10:55 jioni, nderemo na vifijo vilitawala
uwanjani baada ya kombe kutolewa uwanjani, lakini mashabiki wengi wa
Yanga walikerwa na kitendo cha kombe hilo kuwekwa eneo lenye vitambaa
vyekundu na vyeupe.
Baada ya tukio hilo, wachezaji wa Azam walitoka wa
kwanza na kusimama mistari miwili kuwapa heshima wachezaji wa Yanga
wakati wakiingia uwanjani.
Huku mvua ikinyesha, Yanga ilianza mpira kwa kasi
na nusura ipate bao dakika ya tatu, wakati Himid Mao alipopiga pasi ya
chini iliyonasa kwenye maji na kumkuta Ammis Tambwe aliyepiga krosi,
lakini ilikosa mmaliziaji. Azam ilijibu mapigo dakika ya tano, wakati
krosi ya Brian Majwega ilimpita kipa wa Yanga, Dida lakini ilikosa
mmaliziaji.
Yanga ilipata bao la kuongoza dakika 12 kwa mpira
wa adhabu uliopigwa na Coutinho na kumwacha kipa Mwadini Ally asijue la
kufanya. Kabla ya bao hilo beki wa Azam, Mao alimchezea vibaya Tambwe
nje kidogo ya eneo la 18, ndipo Mbrazili huyo alipoonyesha uwezo wake wa
kupiga faulo iliyopita juu ya ukuta wa Azam.
Bao hilo la Yanga lilidumu kwa dakika moja tu,
kabla ya Azam kusawazisha kupitia kwa chipukizi, Bryson Rafael
aliyepokea pasi ndogo ya Domayo akiwa ndani ya eneo la 18 na kupiga
shuti la chini lililompita Dida na kujaa wavuni.
Baada ya bao hilo mashabiki wa Yanga waliokuwa
wamekaa jukwaa pamoja na wale wa Azam waliamua kurejea kwenye jukwaa
lao, huku wakiimba nyimbo za kuikejeli Simba.
Kutokana na mvua kubwa na maji kujaa uwanjani
mwamuzi Jacob Odongo aliwaita manahodha wa timu zote mbili na kukagua
uwanja na kukubali kuendelea na kipindi cha pili.
Yanga ilikosa bao dakika 49, baada ya Aggrey
Morris kuteleza akizuia mpira uliopigwa na Nizar uliomkuta Mrwanda,
lakini shuti lake lilishindwa kulenga lango.
Azam ilimtoa Mwaikimba, Domayo na kuwaingiza
Didier Kavumbagu na John Bocco, mabadiliko yaliyozaa matunda kwa
matajiri hao wa Chamazi.
HII NI KALI YA MWAKA KWA YANGA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 07, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment