Mvua kubwa iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo tangu juzi
imesababisha vifo vya watu watano huku mamia wakikosa makazi baada ya
nyumba zao kubomolewa.
Mvua hiyo iliyofikia kipimo cha milimita 132.5 kwa
mujibu wa vipimo vilivyofanywa katika kituo cha Shule ya Msingi ya
Maktaba, ilisababisha barabara kujaa maji na nyingine kuharibika na
madaraja kadhaa kukatika.
Mkurugenzi Mkuu wa Hali ya Hewa, Dk Agnes Kijazi
alisema jana kwamba kipimo hicho cha mvua ni cha juu mno kulinganisha na
kile cha wastani ambacho ni kati ya milimita 16 na 30.
“Kwa takwimu za mwezi Mei, kiwango hiki hakijawahi
kufikiwa kwa miaka 10 iliyopita.” Alipotakiwa kufafanua miezi mingine,
Dk Kijazi alisema hakuwa na takwimu kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.
Awali, Dk Kijazi alitoa taarifa ikisema mifumo ya
hali ya hewa inaonyesha kuwa “hali ya mvua inatarajiwa kuendelea katika
baadhi ya siku hadi Mei 20, mwaka huu”.
“Mamlaka inaendelea kushauri wakazi wa maeneo hatarishi pamoja na watumiaji wa bahari kuchukua tahadhari,” alisema Dk Kijazi.
Watano wafa
Kutokana na mafuriko hayo, watu watano wakiwamo watoto wawili, walipoteza maisha baada ya kusombwa na maji.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick
alisema waliopoteza maisha ni watoto wawili na mzee mmoja ambao majina
yao hayajafahamika.
“Mtoto mmoja (2) alisombwa na mafuriko katika eneo
Machimbo ya Makangarawe na mzee mmoja alifariki jana baada ya mvua
kunyesha na kujaa ndani ya nyumba yake. Mtoto mwingine ambaye bado
hajapatikana alisombwa na mafuriko pia,” alisema Sadick.
Hata hivyo, habari zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni zilisema kuwa waliopoteza maisha ni watu watano.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alimtaja mtu aliyefariki dunia kuwa ni Shabani Idd (73)
mkazi wa Manzese.
Mvua zaua watano Dar, mamia hawana makazi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 07, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment