Kijana Prims Eliaringa (22), mkazi wa mtaa wa Siara, kata
ya Baraa jijini Arusha, amedai kushambuliwa kwa kuchomwa moto na kukatwa
mapanga na mtu mmoja anayedaiwa kuwa tajiri, aitwaye Donald Mola, pamoja na
mafundi wa ujenzi.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Machi 28, 2025, wakati kijana huyo alipokuwa
akielekea kuomba kazi ya kusaidia mafundi katika nyumba inayojengwa eneo hilo.
Kwa mujibu wa maelezo ya Prims, alipofika kwenye eneo la ujenzi, alikamatwa na
mafundi hao, akatuhumiwa kuwa mwizi na kuanza kushambuliwa bila kufanyiwa
mahojiano yoyote. Anadai alikatwa mapanga na kuchomwa moto katika sehemu
mbalimbali za mwili wake.
Baada ya kushambuliwa, alifungwa kamba na kuwekwa kwenye buti ya gari. Alidai
kusafirishwa hadi kwa mwenyekiti wa mtaa, kisha kwa polisi, na baadaye kutupwa
katika hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu.
Mama mzazi wa kijana huyo, Bi. Rahel Joseph, amesema licha ya kufunguliwa
jalada la kesi lenye kumbukumbu namba ARS/RB/3075/2025, mtuhumiwa hajachukuliwa
hatua yoyote. Anadai kuwa Donald Mola anatumia ushawishi wake wa kifedha
kukwepa mkono wa sheria.
Mwenyekiti wa mtaa huo, James Daniel, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kueleza kuwa alimpokea Prims akiwa katika hali mbaya. Ameonya wananchi kuacha
kujichukulia sheria mikononi.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Justin Masejo,
hazikufanikiwa baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.
No comments:
Post a Comment