Papa Francis amefariki dunia leo Jumatatu ya
Pasaka, Aprili 21, 2025 akiwa na umri wa miaka 88.
Kwa mujibu wa mtandao wa kijamii wa Vatican News,
Papa Francis amefariki dunia akiwa katika makazi yake kwenye nyumba ya
Mtakatifu Marta.
Kiongozi huyu wa Kanisa Katoliki na kiongozi wa
Vatican, alizaliwa Desemba 17, 1936 mjini Buenos Aires, Argentina na kubatizwa
jina la Jorge Mario Bergoglio.
Papa Francis alichaguliwa Jumatano Machi 13, 2013
siku ya pili ya makutano ya makardinali. Alipata ushindi katika duru ya tano ya
upigaji kura.
Katika maisha ya uongozi kiroho, amejulikana kwa
unyenyekevu na msisitizo kuhusu huruma ya Mungu. Kimataifa anatambulika kwa
kuwajali maskini.
Alichagua kuishi kwenye nyumba ya Mtakatifu Marta
(Domus Sanctae Marthae) inayotumiwa na wageni, badala ya kuhamia katika makazi
ya kipapa.
Papa Francis amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya
kudumu ya mapafu, jambo ambalo kwa sehemu limechangia afya yake kuzorota.
Katika miaka ya hivi karibuni alikuwa akipata
matatizo ya mafua, kikohozi, maumivu ya koo na kifua wakati wa baridi.
Pia, maumivu ya magoti na mishipa ya nyonga
yalisababisha mara kwa mara atumie kitimwendo au mkongojo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari
Vatican, Papa Aprili 20, 2025 alikutana katika nyumba ya Mtakatifu Marta na
Makamu wa Rais wa Marekani, James Vance katika mkutano wa faragha uliodumu kwa
dakika kadhaa.
Kwa mujibu wa habari kutoka Vatican, wawili hao
walibadilishana matashi mema katika siku ya Pasaka.
Katika ujumbe wake wa Pasaka kwa mji wa Roma na
dunia kwa mwaka 2025, uliosomwa na mshereheshaji wa Liturujia za Kipapa, Papa
Francis alitoa wito wa kusitishwa mapigano huko Gaza.
Katika ujumbe huo, pia alizungumzia kuhusu amani ya
Ukraine na maeneo ya Afrika. Alitoa mwaliko wa kusaidia wakazi wa Myanmar
waliokumbwa na tetemeko la ardhi.
Papa alisema hakuna amani bila kupokonywa silaha,
akitoa wito wa kuheshimiwa uhuru wa kidini na kuachiwa wafungwa wa vita na wa
kisiasa.
Tangazo la kifo chake
Kwa mujibu wa Vatican, tangazo la Camerlengo
Kardinali Farrell kutoka nyumba ya Mtakatifu Marta imesema:
"Saa 1:35 asubuhi ya leo Jumatatu Aprili 21,
Askofu wa Roma, Francisko alirudi kwenye nyumba ya Baba. Maisha yake yote
yaliwekwa wakfu kwa huduma ya Bwana na Kanisa."
Kardinali Kevin Farrell alitangaza kifo cha Papa
akisema: "Kaka na dada wapendwa ni kwa huzuni kubwa kwamba sina budi
kutangaza kifo cha Baba yetu Mtakatifu Francisko. Saa 1:35 asubuhi ya leo,
(Jumatatu Aprili 21, 2025), Askofu wa Roma, Francisko, alirejea nyumbani kwa
Baba.”
Amesema maisha yake yote yaliwekwa wakfu kwa huduma
ya Bwana na kanisa lake.
“Alitufundisha kuishi maadili ya Injili kwa
uaminifu, ujasiri na upendo wa ulimwengu wote, hasa kwa kupendelea maskini
zaidi na waliotengwa zaidi. Kwa shukrani nyingi kwa ajili ya kielelezo chake
kama mfuasi wa kweli wa Bwana Yesu, tunaiweka roho ya Papa Francisko kwa upendo
wa huruma usio na kikomo wa Mungu mmoja na wa Utatu,” amesema.

No comments:
Post a Comment