Waziri Ndalichako Azindua Baraza La Uongozi La NACTE


Na Regina Mkonde
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako  leo tarehe 9 Agosti, 2018 amelizindua Baraza jipya la Uongozi la Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika jana tarehe 9 Agosti, 2018 katika ukumbi wa mikutano wa NACTE ulioko jijini Dar es Salaam, Prof. Ndalichako alilipongeza baraza lililomaliza muda wake, na kutoa maagizo kwa baraza jipya.

Prof. Ndalichako amelitaka baraza hilo kuendelea kusimamia pamoja na kudhibiti ubora wa elimu inayotolewa na vyuo hapa nchini.

Vile vile, Prof. Ndalichako amelitaka baraza hilo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vyuo vilivyosajiliwa na vitakavyosajiliwa hapa nchini, ili kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wahitimu inakidhi soko la ajira.

Katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako amelitaka baraza jipya la NACTE kuongeza juhudi katika kufanya utafiti wa soko la ajira ili liweze kuwashauri wawekezaji wanaotaka kuanzisha vyuo, kutoa mafunzo yanayokidhi soko la ajira.

Hali kadhalika, Prof. Ndalichako amelitaka baraza la NACTE kusimamia vyema vyanzo vya mapato hasa vya ndani ili liweze kujiendesha kwa ufanisi zaidi.

Sambamba na hilo, ameishauri NACTE kutoa ushauri kwa wanaotaka kuanzisha vyuo, kutoa mafunzo kuhusu sekta zinazotoa ajira kwa sasa, hususani sekta ya kilimo, viwanda, madini na gesi.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi NACTE, Profesa John Kandoro amemhakikishia Prof. Ndalichako kwamba watatekeleza maagizo yake, akisema kuwa, baraza lake litaendelea kufanya tathimini ya ubora wa vyuo pamoja na kuendeleza elimu ya ufundi ili kufanikisha adhma ya serikali ya uchumi wa viwanda. 

Waziri Ndalichako Azindua Baraza La Uongozi La NACTE Waziri Ndalichako Azindua Baraza La Uongozi La NACTE Reviewed by KUSAGANEWS on August 10, 2018 Rating: 5

No comments: