Mfumuko Wa Bei Wa Taifa Umepungua Kufikia Asilimia 3.3

Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Julai, 2018 umepungua hadi kufikia asilimia 3.3 ikilinganishwa na asilimia 3.4  mwezi Juni, 2018.

Hayo yameelezwa  jana na Jijini Dodoma na  Mkurugenzi wa sensa na Takwimu za Jamii, Ofisi ya Taifa ya Takwimu Ephraim Kwesigabo alipokuwa akitoa taarifa  ya mfumuko wa bei kwa mwezi Julai mwaka huu.

Kwesigabo alisema, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018 imepungua ikilinganishwa na kasi ilivyokuwa kwa  mwaka ulioishia mwezi Juni, 2018.

“Kupungua kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018 kumechangiwa hasa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula, ambapo bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei kati ya Julai, 2017 na Julai 2018 ni pamoja na unga wa mahindi kwa asilimia 9.5, mtama kwa asilimia 17.8, unga wa mihogo kwa asilimia 14.1, matunda jamii ya machungwa kwa asilimia 22.2, maharagwe kwa asilimia 5.8 na mihogo mibichi kwa asilimia 12.5,” alifafanua Kwesigabo.

Aliendelea kusema kuwa ni zaidi ya miaka 15 tangu itokee tarakimu kama hiyo ya mfumuko wa bei ambayo iko vizuri kwa uchumi wa nchi.

Aidha alitaja hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya  nchi za Afrika Mashariki kama ifuatavyo; Uganda mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018 umeongezeka hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 2.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018. Kwa upande wa Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018 umeongezeka hadi asilimia 4.35 kutoka asilimia kutoka asilimia 4.28 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2018.

Mfumuko wa bei wa Taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Mfumuko Wa Bei Wa Taifa Umepungua Kufikia Asilimia 3.3 Mfumuko Wa Bei Wa Taifa Umepungua Kufikia Asilimia 3.3 Reviewed by KUSAGANEWS on August 10, 2018 Rating: 5

No comments: