Waziri Mkuu Ataka Wanafunzi Walioanza Shule Kumaliza Pamoja

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha wanafunzi wote wanaoingia kidato wanahitimu masomo yao ya kidato cha nne.

Majaliwa ameyasema hayo jana Alhamisi Agosti 9, alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mnacho iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi akiwa katika ziara yake ya kutembelea jimboni kwake.

“Serikali haitaki kusikia mwanafunzi anaacha shule kwa utoro wala akiacha shule kwa kupata mimba akiwa shuleni badala yake inataka wanafunzi wote wamalize masomo yao salama kwani tumefanikiwa kupunguza baadhi ya changamoto zikiwamo kuajiri walimu wapya ambao wamesambazwa katika shule zao nchi nzima,” alisema.

Hata hivyo, Majaliwa alisema licha ya kuajiri walimu pia serikali imemaliza changamoto ya vitabu kwa kupeleka vitabu vya sayansi ya sanaa katika shule zote za sekondari nchini kwa kupunguza uwiano wa wanafunzi wanaotumia vitabu hivyo ambapo awali kitabu kimoja kilikuwa kinatumika na wanafunzi 10  na kwa sasa kitabu kimoja kinatumika kwa wanafunzi watatu hadi watano.

Alisema mkakati wa serikali kwa siku za usoni ni kuhakikisha kila mwanafunzi anakuwa na kitabu chake cha kujisomea  ili kuwafanya wanafunzi hao kusoma wakiwa huru.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema kuwa Mkoa wa Lindi umekuwa ukifanya vibaya katika mitihani yake ya kitaifa ya darasa la saba na mtihani wa kidato cha nne.

“Katika miaka miwili mfululizo kuanzia mwaka 2015  na 2016  mkoa ulikuwa ukishika nafasi ya mwisho katika mitihani ya kidato cha nne kwa nchi mzima, ambapo kwa  mitihani wa shule ya msingi darasa la saba kwa mwaka jana mkoa ulishika nafasi ya nne kutoka nafasi ya 19 mwaka juzi,” alisema.


Waziri Mkuu Ataka Wanafunzi Walioanza Shule Kumaliza Pamoja Waziri Mkuu Ataka Wanafunzi Walioanza Shule Kumaliza Pamoja Reviewed by KUSAGANEWS on August 10, 2018 Rating: 5

No comments: