Viongozi wa vijiji, vitongoji waongoza kwa rushwa Manyara


Imeelezwa kuwa viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa Mkoani Manyara ndiyo wanaoongoza kwa vitendo vya kuomba na kupokea rushwa wakifuatiwa na polisi, ambao waashika nafasi ya pili kwa mwaka 2017/2018

Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) mkoani Manyara, Isdory Kyando ameyasema hayo jana Agosti 8  mjini Babati wakati akisoma taarifa ya matukio ya mwaka wa fedha wa 2017/2018

Kyando amesema viongozi hao wa vijiji, vitongoji na mitaa walikuwa na malalamiko 47 wakifuatiwa na polisi waliokuwa na malalamiko 42 na nafasi ya tatu ilishikwa na mabaraza ya ardhi ya kata waliokuwa na malalamiko 31

Naibu Mkuu huyo wa Takukuru wa mkoa huo amesema taasisi binafsi zililalamikiwa mara 18 na mahakama yaliripotiwa malalamiko 11

"Kwa mwaka uliopita tulipokea taarifa 315 ambapo kati ya hizo 160 ilikuwa ya rushwa na tukafungua kesi 26 mahakamani na 154 hazikuwa za makosa ya rushwa," amesema Kyando

Amesema kwa mwaka uliopita wamefanikiwa kuanzisha vilabu 225 vya kupinga rushwa kwenye shule za sekondari na msingi na wamefanya tafiti zaidi ya 20 na wakabaini wakuu wa shule kuwachagua wanafunzi wasiokuwa na vigezo

Amesema wanaendelea kutoa elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa ili matukio hayo yamalizike na jamii iweze kupata huduma mbalimbali bila kuombwa au kutoa rushwa kwani ni haki yao ya msingi kupatiwa huduma

"Tunaendelea kutoa elimu kwa watu binafsi na taasisi ili kupambana na matukio ya utoaji rushwa kwani lengo letu ni jamii na viongozi wa taasisi mbalimbali kuelewa hilo," amesema Kyando

Mkazi wa Komoto mjini Babati, Mariam Hassan amesema jamii kwa kiasi kikubwa inachangia matukio ya kutoa na kupokea rushwa kuendelea kuwepo kwani hata suala la kupatiwa huduma bila kutoa chochote wenyewe hutoa bila kuombwa

"Mara nyingi watu hutanguliza fedha kama ni ofisi za vijiji au polisi japokuwa wapo wanaodaiwa rushwa kabla ya kupatiwa huduma japokuwa ni mara chache kwenye hilo," amesema Hassan

Viongozi wa vijiji, vitongoji waongoza kwa rushwa Manyara Viongozi wa vijiji, vitongoji waongoza kwa rushwa Manyara Reviewed by KUSAGANEWS on August 09, 2018 Rating: 5

No comments: