Profesa Ndalichako ataka maktaba wilayani


Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako ameitaka bodi ya huduma za maktaba kupeleka huduma hizo kwenye wilaya

Amesema jambo hilo litachangia kuongeza idadi ya Watanzania watakaohamasika kusoma na kutumia huduma za maktaba

Profesa Ndalichako ametoa agizo hilo leo Agosti 7 wakati akizundua bodi mpya ya huduma za maktaba inayoongozwa na mwenyekiti wake, Profesa Rwekaza Mukandala

Katika kufanikisha hilo Profesa Ndalichako amewataka wakurugenzi wa halmashauri kutenga maeneo au chumba maalum kwa ajili ya kujisomea.

 Amesema uwepo wa huduma za maktaba karibu na wananchi kutasaidia kuwavuta watu wengi kutafuta maarifa hasa katika kipindi hiki ambacho nchi ina dhamira ya kufikia uchumi wa viwanda

"Tunapotaka kufikia uchumi wa viwanda lazima watu wasome, wavune ujuzi kutoka kwenye vitabu na machapisho na hakuna sehemu nyingine ya kupata zaidi ya maktaba,"amesema.

 Amesema Serikali itaendelea kuijengea uwezo taasisi hiyo ili kuboresha huduma za maktaba kwa Tanzania Bara

Pia aliisisitiza bodi hiyo kuhamasisha utamaduni wa kusoma pamoja na kuweka machapisho yanayogusa nyanja zote hususani viwanda na makundi ya aina tofauti hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchumi wa viwanda

Amesema tafiti nyingi zinategemea uwepo wa maandiko hivyo maktaba ni nyezo muhimu kwa watafiti

Amesema bodi hiyo ina mchango mkubwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuhakikisha uwepo wa vitabu na huduma za maktaba zinawafikia Watanzania wengi

"Maktaba ni kisima cha ujuzi, maarifa na kisima ambacho kinawawezesha watu kupata vitu ambavyo hawawezi kupata sehemu nyingi,"amesema

Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi hiyo Profesa Mukandara amesema anatambua umuhimu wa jukumu walilopewa na watafanyakazi kwa ufanisi mkubwa

"Tumechukua maelekezo yako na tunaenda kuyafanyia kazi kwa kuwa tunafahamu umuhimu wa huduma za maktaba kwa taifa,"amesema

Profesa Ndalichako ataka maktaba wilayani Profesa Ndalichako ataka maktaba wilayani   Reviewed by KUSAGANEWS on August 07, 2018 Rating: 5

No comments: