Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert
Chalamila amekabidhiwa ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla huku
akijiapiza kuwa yuko tayari kutumbuliwa na Rais kama viongozi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) mkoani humo, hawatakubali kuondoa makundi na kupoteza tena
Jimbo la Mbeya Mjini.
Chalamila alitoa kauli hiyo wakati
wa makabidhiano hayo jana na kudai kuwa kwa mtazamo wake anaona jimbo hilo kwa
sasa lipo wazi na linaweza kurejea katika himaya ya CCM katika uchaguzi mkuu
ujao wa mwaka 2020.
CCM ililipoteza kwa mara ya kwanza
jimbo hilo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, Polisya Mwaiseje (NCCR-Mageuzi)
alipomshinda Bruno Mpangala, lakini ikalirejesha mwaka 2000 kupitia kwa Benson
Mpesya.
Mwaka 2010, Mpesya aliangushwa na
Joseph Mbilinyi 'Sugu' (Chadema) anayeendelea kuliongoza hadi sasa.
Katika makabidhiano hayo, Chalamila
alisema kuwa pamoja na mtazamo wake huo wa uwezekano mkubwa wa kulirejesha CCM
jimbo hilo, wanachama wa CCM wasishangae kushindwa tena ikiwa wataendelea na
makundi makubwa yaliyo ndani ya chama hicho.
Alisema amekuwa akifuatilia migogoro
ya CCM Mbeya tangu alipokuwa Iringa na amebaini kuna makundi makubwa ambayo
yanaweza kukigharimu chama hicho.
“Endapo nitaondolewa kwa sababu ya
CCM kupoteza jimbo hili, nitarudi kulima, nitamshukuru Rais na nitamwambia kuwa
sijasikitika," Chalamila alisema na kuongeza:
"Kama mtataka ushirikiano wa
kujenga, mimi kama kamisaa wa chama, nitawapa lakini kama ni ushirikiano wa
kuvurugana sitawapa."
Aliongeza kuwa msimamo wake ni
kufanya kazi bila kuingiliwa na kiongozi yeyote na yeyote atakayetaka kuingilia
majukumu yake atamtaka kusoma katiba na miongozo ya chama.
Chalamila alimshauri Mwenyekiti wa
CCM Mkoa wa Mbeya, Jacob Mwakasole na timu yake kuhakikisha wanapambana na
kuyaondoa mapema makundi yaliyokivuruga chama hicho.
Alisema kuwa atakuwa tayari kutoa
ushauri na kama wataona ushauri wake haufai, atawaacha na hatawaingilia katika
uamuzi wao.
Kiongozi huyo wa serikali aliongeza
kuwa kwa muda mrefu wananchi wa Mkoa Mbeya wamefarakanishwa kwa itikadi za
kisiasa zilizokuwa zinasababishwa na baadhi ya viongozi.
Alimpongeza Makalla kwa jitihada
alizozionyesha kwenye utatuzi wa migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya
mkoa huo, hasa Mbarali na Rungwe.
Awali, Makalla ambaye amehamishiwa
Mkoa wa Katavi, alimweleza Chalamila kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja na
miezi minne, alikuwa anapambana na migogoro ya ardhi ambayo ndiyo ilikuwa
changamoto kubwa mkoani humo.
Alisema baadhi ya migogoro
alishaimaliza ikiwamo ya wananchi waliohamishwa wakati wa upanuzi wa Hifadhi ya
Taifa ya Ruaha. Wananchi hao walikuwa wanalalamika kupunjwa malipo ya fidia.
“Nakuhakikishia kuwa tumeshirikiana
na wakuu wa wilaya pamoja na viongozi wengine wakiwamo wa dini kumaliza baadhi
ya changamoto, lakini nitakukabidhi baadhi ya migogoro ya ardhi kwa maandishi
ili uendelee kuitatua,” alisema.
Makalla aliwataka wananchi na
viongozi wa Mbeya kumpa ushirikiano Chalamila kama walivyofanya kwake wakati
akiuongoza mkoa huo unaosifika kwa uzalishaji wa nafaka.
Mkuu Mpya wa mkoa wa Mbeya ajiapiza kumng'oa Sugu jimboni 2020
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 07, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment