Kibatala asema Mahakama ina mamlaka kuahirisha kesi ya kina Mbowe


Wakili Peter Kibatala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa ina mamlaka ya kuiahirisha kesi ya jinai namba 112/2018 kwa kipindi kisichozidi siku 30 kwa kuwa washtakiwa wapo nje kwa dhamana

Kibatala ameyaeleza hayo leo Agosti 21 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wakati wa usikilizwaji wa maombi ya viongozi tisa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo uchochezi, kufanya maandamano yaliyohamasisha chuki, kuhamasisha maandamano, mnamo Februari 16 jijini Dar es Salaam.
 Wakili Kibatala  ameomba kesi hiyo iahirishwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa

Wakili Kibatala, alidai kuwa kifungu cha 225(1) (2) sura ya 20 ya sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ambacho ndio wametumia kuleta maombi hayo kinaipa mahakama hiyo mamlaka ya kufanya hayo

Katika maombi yao wanaomba Mahakama ya Kisutu iridhie kuahirisha usikilizwaji wa kesi ya jinai namba 112/2018 ili kutoa nafasi kwa Mahakama ya Rufaa kuisikiliza na kutoa uamuzi katika maombi ya kusimama kwa kesi ya msingi iliyopo Mahakama ya Kisutu na rufaa namba 215/2018

Kibatala amedai kuwa rufaa hiyo inatokana na maamuzi ya Mahakama Kuu ya kuyatupilia mbali maombi yao ya marejeo

Amedai kuwa kifungu hicho kinaipa Mahakama mamlaka ya kuahirisha usikilizwaji wa kesi hiyo ya jinai namba 112/2018 kwa kipindi kisichozidi siku 15 iwapo mshtakiwa atakuwa ndani na kwa kipindi kisichozidi siku 30 iwapo mshtakiwa ama washtakiwa watakuwa nje kwa dhamana

Akijibu hoja hizo za wakili Kibatala, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi amedai kuwa maombi hayo ya utetezi yanakosa baraka za kisheria na hata miguu ya kisheria ya kusimama mbele ya mahakama hiyo

Wakili Nchimbi aliiomba mahakama itupilie mbali maombi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi kwa sababu yanakosa msingi wa kisheria

Nchimbi amedai kuwa hati ambayo wamewasilisha wao kama upande wa mashtaka katika kesi hiyo Agosti 14, mwaka huu inakidhi vigezo vyote vya kisheria vya uandishi wa hati kinzani

Amedai kuwa maombi hayo ya upande wa utetezi ni maombi ambayo yana lengo la kuchelewesha kesi

Aliongeza kudai kuwa katika hatua hiyo ya upande wa utetezi hakuna chochote kipya ambacho wamewasilisha mahakamani kwa kuwa mara kadhaa wamekuwa wakiwasilisha maombi tofauti tofauti na mahakama imekuwa ikitoa maamuzi ikiwamo kuyatupilia mbali

Baada ya kusikiliza pande zote mbili Hakimu Mashauri aliiahirisha usikilizwaji wa maombi hayo hadi Agosti 23, mwaka huu ambapo atatoa uamuzi kesi hiyo iahirishwe ama la

Katika kesi ya msingi, Hakimu Mashauri pia aliiahirisha hadi Agosti 23, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa
Washtakiwa wanaokabiliwa katika kesi hiyo ni viongozi tisa wa Chadema akiwamo Freeman Mbowe

Mbali na Mbowe wengine ni naibu katibu mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na naibu katibu mkuu bara na Mbunge wa Kibamba John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee na  Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya

Wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji

Hata hivyo wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo ya utetezi, washtakiwa Halima Mdee na Esther Bulaya hawakuwepo mahakamani

Waliwakilishwa na wadhamini wao ambapo walidai kuwa wapo bungeni katika kamati ya kudumu ya sheria ndogo

Maelezo hayo ya wadhamini yalisababisha Hakimu atoe onyo la wabunge hao kutohudhuria mahakamani

Hakimu Mashauri amesema anafahamu dhamana ni haki ya kikatiba lakini mahakama imegundua kuwa kuna mchezo wanaufanya hivyo mchezo huo utawagharimu kwa sababu atakuja kuwafutia dhamana wote na wakakaa ndani hadi kesi iishe

Kibatala asema Mahakama ina mamlaka kuahirisha kesi ya kina Mbowe Kibatala asema Mahakama ina mamlaka kuahirisha kesi ya kina Mbowe Reviewed by KUSAGANEWS on August 21, 2018 Rating: 5

No comments: