Ripoti ya Taasisi ya Twaweza iliyotolewa juzi jijini Dar es
Salaam imeibua mjadala mzito, huku wengi wakihoji sababu ya viongozi wa
kuchaguliwa kupoteza umaarufu
Utafiti huo, uliohusisha takwimu zilizokusanywa kutoka kwa
watu 1,241 waliohojiwa kutoka Tanzania Bara mwezi Aprili, unaonyesha uungwaji
mkono wa Rais John Magufuli umeshuka kutoka asilimia 96 mwaka 2016 mpaka
asilimia 55 mwaka 2018, ikiwa ni kiwango cha chini kabisa kuwahi kutokea kwenye
historia ya nchi
Hata hivyo, utafiti huo unaonyesha kuwa kama uchaguzi
ungefanywa wakati huo, asilimia 55 ya wananchi wangempigia kura. Vilevile
umeonyesha bado wananchi kwa kiasi kikubwa wanaendelea kuunga mkono wagombea wa
CCM
“Zaidi ya nusu wangewapigia kura wagombea wa CCM wa udiwani
(asilimia 51), wabunge (asilimia 51), na urais (asilimia 55). Uungwaji mkono wa
CCM kama chama umeendelea kuwa imara kiasi kwenye miaka ya hivi karibuni kukiwa
na asilimia 63 ya wananchi wanaosema wako karibu na CCM mwaka 2017
ukilinganisha na asilimia 58 mwaka 2018,” imeonyesha sehemu ya utafiti huo
Wakizungumza katika hafla ya kuwasilisha ripoti hiyo, baadhi
ya wachangiaji walielezea sababu za kushuka huko huku pia wakitoa suluhisho
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Vicencia Shule
alihusisha kushuka huko na suala la kijinsia, akisema wanawake ambao ndiyo
wapigakura wengi wamepuuzwa
Alisema licha ya kupuuzwa, utafiti huo umeonyesha kuamka kwa
wanawake hasa kwenye suala la maandamano
“Kwenye suala la maandamano, ufahamu wanawake na wanaume na
wanaume kitakwimu hawakupishana sana. Wanaume ni asilimia 43 na wanawake ni
asilimia 41. Pamoja na kuogopa vurugu, wanawake wameelewa kwamba yale madai
yaliyoleta maandamano ni madai yao,” alisema Dk Shule
Mbali na wanawake, Dk Shule alisema uelewa wa wanaume
umeshuka kwenye matatizo ya kijamii, wakati wao ndiyo wameshikilia uongozi wa
Dola
“Wanaume wa nchi hii ndiyo waliojitwalia madaraka ya
kuongoza nchi bila kujali idadi ya wanawake. Kitu kingine kizuri zaidi ni
umaarufu wa Rais unazidi kushuka. Wananchi wameelewa kipi kinatekelezeka na
kipi hakitekelezeki,” alisema
Alisema kumekuwepo na tishio la viongozi kupiga wanawake,
jambo linalosababisha kushuka kwa kukubalika kwao kwa kuwa wanawake ni wengi
katika idadi ya wapiga kura
“Hakuna mtu atakukubali kama unapiga mashangazi, hakuna mtu
atakupenda kama unatisha wanawake. Kwa hiyo hii ni ‘wake-up call’ kwa
mwenyekiti wa chama, kwamba matendo yake kwa wapigakura ambao wengi ni wanawake,
yanathibitisha wazi kuwa umaarufu wake unashuka kwa kuwakosea haki hata
kuwanyima fursa ya kushika dola,” alisema
Ripoti ya Twaweza ilivyozua mjadala, sababu za viongozi kupoteza umaarufu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 07, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 07, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment