Simba
SC ndiyo mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Hiyo ni baada ya
waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC kulitema rasmi taji hilo leo, kufuatia
kufungwa mabao 2-0 na wenyeji, Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Kwa maana
hiyo, pointi 65 ambazo wamejikusanyia Simba SC hadi sasa zinawatosha kuitwa
mabingwa, kwani Yanga wenye pointi 48 kwa sasa baada ya kucheza mechi 25, hata
wakishinda mechi zao zote zilizosalia watafikisha pointi 63 tu.
Yanga
inauachia ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kukaa nao kwa misimu mitatu mfululizio
wakati, Simba SC inatwaa taji la kwanza la ligi hiyo tangu mwaka 2012
walipochukua kwa mara ya mwisho.
Katika
mchezo wa leo mabao ya Tanzania Prisons yamefungwa na Eliuter Mpepo kwa penalti
dakika ya 58 baada ya kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko kuushika mpira kwenye
boksi na Salum Bosco aliyefunga la pili dakika ya 85 akitumia udhaifu wa mabeki
wa Yanga.
Matokeo haya
pia yanamaanisha Yanga SC hawatashiriki michuano ya Afrika mwakani, kwani
tayari wametolewa pia na kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
maarufu kama Azam Sports Federation (ASFC) katika hatua ya Robo Fainali
tu.
Mechi
nyingine ya Ligi Kuu leo, bao pekee la Vincent Philipo dakika ya 45 na ushei
limeipa Mbao FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa CCM Kirumba mjiniu
Mwanza.
Kwa ushindi
huo, Mbao FC inafikisha pointi 27 baada ya kucheza mechi 27 na kupanda kwa
nafasi moja hadi ya 13, wakati Ndanda FC inabaki nafasi ya 15 kwa pointi zake
23 za mechi 28 kwenye Ligi ya timu 16, ambayo timu mbili zitashuka wiki mbili
zijazo.
Kikosi cha
Tanzania Prisons kilikuwa; Aaron Kalambo, Michael Ismail, Laurian Mpalile,
Nurdin Chona, James Mwasote/Vedastus Mwahiambi, Jumanne Elfadhil, Benjamin
Asukile, Cleophace Mkandala/Adam Kimbongwe, Mohammed Rashid, Ramadhani
Ibata/Salum Bosco na Eliuter Mpepo.
Yanga SC;
Benno Kakolanya, Juma Abdul, Emmanuel Martin, Pato Ngonyani, Abdallah Shaibu
‘Ninja’, Maka Edward, Paulo Godfrey/Amissi Tambwe, Thabani Kamusoko, Yohanna
Nkomola, Matheo Anthony na Baruan Akilimali/Yussuf Suleiman.
Yanga yakabidhi kombe ligi kuu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 10, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment