Wakuu wa Wilaya, wabunge waliowachoma sindano mabinti watakiwa kuomba radhi


Wabunge wameitaka Serikali kuchukua hatua ikiwamo kuwataka wanasiasa walioonekana wakiwachoma sindano ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi, kuomba radhi na kuwalipa fidia watoto hao

Hata hivyo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kilichofanyika ni majaribo huku akikiri kushika sindano kama si mtaalamu ni makosa

Hayo yamejitokeza leo Mei 3, 2018 bungeni mjini Dodoma wakati wabunge wakiomba mwongozo wa Spika, wakitumia kanuni ya 67 (8) ya jambo lililotokea hivi karibuni

Aliyeanzisha alikuwa mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Anatropia Theonest aliyehoji kuwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, wamejitokeza madaktari wa ghafla wakiwamo wakuu wa wilaya na wabunge, wakichanja watoto

“Sasa nimepata taharuki, sisi kama hatuna taaluma, tunachomaje sindano, nimesikia waziri ametoa kauli lakini haitoshi, nimesoma miiko ya madaktari hairuhusu, nimesoma miiko ya wauguzi hakuna,” amesema

Katika kusisitiza hilo, Theonest amesema;  “Madaktari wamevunja miiko, wauguzi wamevunja miiko na wanasiasa hao wamevunja maadili yao. Naomba hao watu waliochoma sindano wawaombe radhi na watoto wapewe fidia na mabaraza husika yanachukua hatua gani katika hilo?”

Mbunge mwingine wa Viti Maalum (Chadema), Anna Gidarya alimuunga mkono Theonest akisema;  “Huwezi kwenda tu kumchoma, chanjo ndizo zinaleta matatizo hata sisi wataalamu tunajua.”
Akitoa majibu ya miongozo hiyo, Spika Job Ndugai amesema, “Tunawaachia Serikali walifuatilie.”

Waziri  Mwalimu alijibu miongozo hiyo akisema

“Nakiri, uchomaji wa sindano una taratibu zake, huwezi kujichomea ovyo ovyo, nawahakikishia Mshana na Mlinga hawakuwachoma chanjo watoto husika ila walifanya kama majaribio.”

Mwalimu amesema ametoa maagizo kwa waganga wa mkoa na wilaya na kuwaeleza kuwa hata kushika sindano ni makosa

Wakuu wa Wilaya, wabunge waliowachoma sindano mabinti watakiwa kuomba radhi Wakuu wa Wilaya, wabunge waliowachoma sindano mabinti watakiwa kuomba radhi Reviewed by KUSAGANEWS on May 03, 2018 Rating: 5

No comments: