Wakili wa Seth, Rugemalira ageuka mbogo mhakamani


Didas Respicius, wakili wa utetezi katika kesi inayomkabili Harbinder Seth na mfanyabiashara James Rugemalira, amewasilisha malalamiko Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa washtakiwa hao wamefikisha mwaka mmoja  gerezani na upelelezi wa kesi inayowakabili bado haujakamilika.

 Wakili huyo ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 24, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Iman Mizizi kueleza upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika

Didas amedai  kuwa washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Juni 19, 2017 wakiwa na mashtaka ambayo yanadhaminika lakini wakiwa katika kuwasilisha maombi ya dhamana, walibadilishiwa mashtaka ambayo hayana dhamana

Amesema tangu mwaka jana hadi sasa upande wa mashtaka unadai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, kwamba  kuwa kwa mujibu wa hati ya mashtaka washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo, mwaka 2013. Amebainisha kuwa walifikishwa mahakamani miaka minne baadae lakini mpaka sasa bado inadaiwa upelelezi haujakamilika.

 Ameomba upande wa mashtaka ufanye kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na Katiba kwa kujali haki za washtakiwa ili kesi iendelee mbele, kuutaka upande wa mashtaka ndani ya siku 14 ueleze upelelezi umekamilika,  kama haujakamilika washtakiwa waachiwe huru

Wakili Mizizi alidai suala la Seth kupatiwa matibabu bado  linashughulikiwa na kwamba wanasubiri jopo la madaktari litakapokamilika atapatiwa matibabu

Amesema Katiba  ndiyo inayotumika kutunga sheria na ndiyo iliyotumika kuwafunguliwa mashtaka washtakiwa 

Baada ya kusikiliza hoja zote, Hakimu Shaidi amesema amezingatia hoja zote na akashauri  upande wa utetezi kupeleka maombi Mahakama Kuu kwa ajili ya kupata maelekezo ya sheria ambazo zinalalamikiwa na zile zinazowafunga mikono

Hakimu Shaidi aliiahirisha kesi hiyo hadi  Juni 7, 2018 kwa ajili ya kutajwa

Sethi na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi,  kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kusababisha hasara ya Dola 22 milioni  za Marekani.
Wakili wa Seth, Rugemalira ageuka mbogo mhakamani Wakili wa Seth, Rugemalira ageuka mbogo mhakamani Reviewed by KUSAGANEWS on May 24, 2018 Rating: 5

No comments: