Zaidi ya mabaharia 800 kutoka Zanzibar waliokuwa wakifanya
kazi katika meli mbalimbali nje ya Tanzania, wamesimamishwa wakihusishwa na
usafirishaji wa dawa za kulevya katika meli hizo.
Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki iliyopita na mkurugenzi wa
kampuni ya ubaharia ya Danaos, Ali Mzee Yussuf
Yussuf aliyasema hayo wakati wa mafunzo maalumu yaliyowashirikisha
mabaharia mbalimbali visiwani hapa yenye lengo la kupiga vita matumizi na
kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya
Alisema awali mabaharia kutoka katika kampuni hiyo walikuwa
zaidi ya 1,000 lakini kwa sasa wamebaki 200 baada ya wengi wao kukamatwa kwa
madai ya matumizi na kusafirisha dawa za kulevya
“Hali hii imekuja baada ya wamiliki wa kampuni za meli
husika kuona kuwa mabaharia wetu mara kwa mara hukamatwa kwa kujihusisha na
usafirishaji wa dawa za kulevya, hivyo wakaona ni bora kupunguza idadi kutoka
kwetu ili kuzinusuru meli zao kuingia katika matata ya usafirishaji dawa hizo,”
alisema Yussuf.
Alisema ni ukweli usiopingika kuwa kuna baadhi ya mabaharia
kutoka kampuni yao wamekuwa wakikamatwa na dawa za kulevya kutokana na tamaa
zao binafsi, lakini kampuni haihusiki
Mkurugenzi huyo alisema kutokana na hali hiyo wamedhamiria
kutoa mafunzo kwa baadhi ya mabaharia wa Zanzibar, ili kuwaonyesha hasara
watakazozipata wakikamatwa na dawa hizo
“Kwa sasa kupitia chuo chetu cha ubaharia Zanzibar, tumeweka
utaratibu maalumu kwa mabaharia wote kutoka hapa lazima wapatiwe elimu ya
athari za dawa za kulevya. Mbali na hilo tutafanya uchunguzi maalumu juu yake
ili kuona tabia zake kama zinafaa kuwa naye au la, lengo ni kuona kampuni yetu
inazidi kupata sifa duniani,” alisema Yussuf
Naye ofisa wa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA), Khamis
Mohamed Ali alisema kitendo cha mabaharia kujihusisha na usafirishaji dawa za
kulevya katika meli hakikubaliki kwa mujibu wa taratibu za kazi.
Ali alisema kitendo
hicho kinaitia aibu kubwa nchi kwa kuonekana inajihusisha na vitendo hatari vya
dawa za kulevya.
Alisema wao kama Serikali mara nyingi wamekuwa wakifanya
kazi na kampuni hiyo lengo ni kuona wanatekeleza majukumu yao vizuri, ila ni
jambo la kushangaza baadhi yao wamekuwa wakijihusiha na usafirishaji wa dawa za
kulevya.
Usafirishaji dawa za kulevya wawanyima ajira mabaharia
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 13, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment