Uganda kulipa mshahara kwa kuhesabu siku kazini


Serikali inatarajia kuanza utaratibu wa kuwalipa mshahara watumishi wake kwa kuhesabu siku walizofanya kazi badala ya huu wa sasa wa kuwahakikishia malipo mwishoni mwa mwezi, ofisa mmoja alisema Jumanne

Profesa Ezra Suruma, ambaye ni Mkuu wa kitengo cha usambazaji vifaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu (OPM), alisema kwa kuanzia wanafunga vifaa vya kielektroniki vya uandikishaji katika taasisi za afya kwa umma na elimu ili kufuatilia wafanyakazi wa idara ya afya na walimu wanavyoingia na kutoka vituoni

Profesa Suruma alisema mishahara ya watumishi wanaokosekana kazini itapunguzwa kwa idadi ya siku ambazo hakuwepo kazini
“Wiki iliyopita, tulikuwa Jinja kwa ajili ya mkutano na viongozi wa serikali za mitaa kwa ngazi za wilaya na tuliambiwa kwamba baadhi ya wilaya haziwalipi tena watumishi wanaokosekana kazini. 

Tunataka wilaya nyingine ziige kwa sababu hakuna mchezo tena,” alisema
Wilaya zilizoanza utekelezaji wa kulipa watumishi wao kwa kuzingatia siku walizofanya kazi ni Kaliro, Kayunga, Buvuma, Bulambuli, Bugiri na Bududa. Wilaya hizo ziko Mashariki mwa Uganda
Matibabu kwa vitambulisho

Mabadiliko mengine ya kisera ni katika matibabu ambapo Serikali iko katika hatua za mwisho za maandalizi ya kutekeleza pendekezo linalotaka watu wenye vitambulisho vya taifa (IDS) pekee ndio wapatiwe huduma za afya katika vituo vya afya vya umma, gazeti la The Monitor limebaini

Waziri wa Afya Jane Aceng Jumatatu alithibitisha kwamba wanajenga mfumo wa kidigitali ili pamoja na mambo mengine, uwawezeshe wafamasia kutowapatia dawa wagonjwa ambao hawana vitambulisho vya taifa

“Hivi sasa tunafanyia kazi programu hiyo ya kuhifadhi taarifa. Bado tunafanyia kazi pamoja na kukusanya raslimali kwa vile tunataka usambazwe nchi nzima,” alisema Dk Aceng katika mahojiano
Faida za mpango

Maofisa wa serikali wanatumai kwamba mpango huo utafanya iwe rahisi kwao kupata rekodi za wagonjwa, kuwa na hesabu inayoeleweka ya idadi ya wagonjwa na kuwa na mfumo mzuri wa ufuatiliaji, uwajibikaji na matumizi ya dawa zilizosambazwa katika huduma za umma

Mpango huo wa Serikali umepokewa kwa hisia tofauti na wanaharakati watetezi wa haki za afya, wataalamu wa tiba na wananchi

Wakati Rais wa Chama cha Madaktari Uganda, Dk Ekwaro Obuku alikaribisha wazo hilo baadhi ya wananchi waliukosoa na wakaufananisha na hukumu ya vifo vya halaiki.
Uganda kulipa mshahara kwa kuhesabu siku kazini Uganda kulipa mshahara kwa kuhesabu siku kazini Reviewed by KUSAGANEWS on May 23, 2018 Rating: 5

No comments: