Serikali imesema ipo haja ya
kuridhia mkataba wa kupambana na silaha za baolojia na sumu ili kuweza kutoa
fursa kwa wataalamu mbalimbali nchini katika kuwajengea uwezo wa kukabiliana na
athari za mashambulizi ya silaha za sumu na kibaoloji.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 11,
2018 na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Dkt. Hussein Mwinyi
Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 28 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu la akijibu swali la Mbunge wa
viti maalum Jasson Rweikiza aliyetaka kujua ni kwa nini Tanzania haijajiunga na
mkataba wa kupambana na silaha za sumu (Biological Weapons Convention).
"Tanzania ilisaini mkataba wa
kupambana na silaha za baolojia na sumu tarehe 1 Agosti, 1972 lakini mpaka sasa
haijaridhia mkataba huo, kutoridhiwa kwa mkataba huo kulitokana na kutoonekana
athari zake za moja kwa moja kwa wakati huo ambapo matumizi salama ya mkataba
ikiwemo utafiti wa magonjwa ya binadamu, wanyama na mimea yameendelea kufanyika
nje ya mkataba huo. Changamoto zinazotokana na matishio mbalimbali ikiwemo
ugaidi, zimesababisha hitaji la kuridhiwa kwa mkataba huo na kutekelezwa kwa
vitendo baada ya kutungiwa sheria",
amesema Dkt. Mwinyi.
Pamoja na hayo, Dkt. Mwinyi
ameendelea kwa kusema
"serikali inafahamu madhara
yaliyopo hivi sasa ya kutoridhiwa kwa mkataba huo ikiwemo Tanzania kuwa katika
kundi dogo la nchi ambazo hazijaridhia mkataba huo kama vile Haiti, Jamhuri ya
Afrika ya Kati, Misri, Somalia na Syria ambapo Tanzania kuwepo katika kundi
hilo hakutoi taswira nzuri kwa jamii ya Kimataifa kwani kati ya nchi hizo
nyingi zina migogoro ya muda mrefu ya ndani....
kuwanyima fursa wataalamu wetu
kupata mafunzo mbalimbali yanayotolewa katika kujenga uwezo wa kukabiliana na
athari za mashambulizi ya silaha za sumu na kibaolojia na pia kunanyima fursa
kwa wataalamu na viongozi wa kitanzania kushiriki kwenye uongozi wa taasisi
mbalimbali za kimataifa zinazosimamia sheria za silaha za kibaolojia na
sumu".
Kwa upande mwingine, Dkt. Mwinyi
amesema teyari waraka umeshaandaliwa na muda si mwingi utapelekwa Bungeni kwa
ajili ya kuridhiwa ambapo ameahidi mpaka kufikia Septemba 2018 utakuwa
umeshawasilishwa.
Tanzania kupambana na silaha za baolojia na sumu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 14, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment