Simanzi ilitawala jana wakati
majeneza yenye miili ya maofisa watatu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),
waliofariki dunia pamoja walipoagwa na wakazi wa Dar es Salaam kwenye Viwanja
vya Karimjee
Tukio hilo liliibua vilio na
simanzi na hata baadhi ya waombolezaji kusikika wakisema, “wamefariki wakiwa
bado vijana.”
Maofisa hao waliofariki dunia
Jumatatu wiki hii ni meneja wa Tafiti na Miradi, Martin Masalu; kaimu
mkurugenzi wa Tafiti, Said Moshi na kaimu mkurugenzi wa Uhusiano, Zacharia
Kingu
Watatu hao walifariki kwa ajali ya
gari katika Kijiji cha Msoga, Chalinze mkoani Pwani wakati wakitoka jijini
Dar es Salaam kwenda Dodoma kwa safari ya kikazi ambapo gari walilokuwa
wakisafiria mali ya Serikali liligonga lori na kusababisha vifo vyao na wengine
wawili kujeruhiwa
Katika tukio hilo, waziri wa
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage aliongoza mamia ya wakazi wa
Jiji la Dar es Salaam kuaga miili ya maofisa hao kuanzia saa 5.30 asubuhi na
baadaye mazishi ya Kingu yaliyofanyika mchana kwenye makaburi ya Kinondoni
Mwili wa Masalu ulitarajiwa
kusafirishwa jana jioni kwenda Mazimbu mkoani Morogoro ambako utazikwa leo
wakati ule wa Moshi utazikwa Monduli mkoani Arusha. Ndugu, jamaa na marafiki
walianza kuwasili katika viwanja hivyo kuanzia saa 3.00 asubuhi
Mbali ya Mwijage pia walikuwepo
maofisa wa Serikali, wawekezaji na wadau wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania
(TPSF) walioongozwa na mkurugenzi mtendaji, Godfrey Simbeye
Hata hivyo, tofauti na
ilivyozoeleka kwa waombolezaji katika misiba ya Kikristo, hawakupata fursa ya
kuiona miili ya wapendwa wao kwa mara ya mwisho kwa kuwa majeneza hayo
hayakufunguliwa
Awali, tangazo lilitolewa
likiwaeleza waombolezaji kuwa hawatafunguliwa majeneza hayo kutokana na
ushauri uliotolewa na madaktari. Kutokana na tangazo hilo, waombolezaji
walitakiwa kupita na kutoa heshima za mwisho mbele ya majeneza, lakini
hawakuiona miili ya marehemu
Umahiri wao watajwa
Akizungumza kabla ya kuaga,
Mwijage alisema kituo hicho kimepata pigo kwa kupoteza vijana mahiri kazini
“Nilipigiwa simu Jumatatu nikiwa
Nzega, nilikuwa safarini kutoka Mwanza kwenda Dodoma nikaambiwa hawa vijana
wamefariki, nilisikitika sana,” alisema
Mwijage alisema wamepoteza vijana
wachapakazi ambao walifanya kazi hadi usiku ili kuhakikisha kituo hicho
kinatekeleza majukumu yake kwa ufanisi
“Tumepoteza wapiganaji waliokuwa
tayari kwa mapambano katika utekelezaji wa sera ya ujenzi wa viwanda,”
alisema
Aliwataka wawekezaji kutovunjika
moyo kwa kuondokewa na vijana hao akisema kituo kitaendelea kuboresha huduma
zake
Mkurugenzi mtendaji wa TIC,
Geoffrey Mwambe alisema amepoteza vijana ambao walikuwa na mchango mkubwa
katika kituo hicho
Alisema wakati wa uhai wao
walichapa kazi kwa weledi na uaminifu hasa katika kipindi hiki ambacho
Serikali inavutia wawekezaji kuja nchini
Mkurugenzi wa TPSF, Simbeye
alisema alikuwa akifanya kazi kwa karibu na vijana hao na zilikuwa rahisi
kutokana na umariri wa wafanyakazi hao
“Nimekuwa karibu na vijana hawa
kama kiongozi wa sekta binafsi, tulishirikiana, walikuwa wachapakazi,”
alisema
Katibu mtendaji wa Baraza la
Biashara Tanzania (TNBC), Raymond Mbilinyi alisema aliwahi kufanya kazi na
vijana hao wakati huo akiwa TIC na kwamba, anaukumbuka vizuri mchango wao
“Hata nilipoondoka nimeendelea
kushirikiana nao, tumepata pigo kuwapoteza,” alisema. Wengine waliohudhuria
mazishi hayo ni waliowahi kuwa wakurugenzi watendaji wa kituo hicho, Emmanuel
Ole Naiko na Clifford Tandali ambaye sasa ni katibu tawala wa Mkoa wa Morogoro
Mazishi ya Kingu
Mazishi ya Kingu yalifanyika jana
kuanzia saa 7.30 mchana hadi saa 8.40 mchana katika makaburi ya Kinondoni
ambayo yalihudhuriwa pia na Mwijage
Mazishi hayo yaliongozwa na
mwinjilisti Ernest Huruma wa KKKT Usharika wa Ununio aliyesema katika
mahubiri yake kuwa, “maisha ni mafupi, binadamu tuishi tukijua kifo kinaweza
kutukuta wakati wowote na mahali popote.”
|
Simanzi ilivyotawala miili ya maofisa TIC ikiagwa Dar
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 24, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment