Hatima ya wana CCM waliotajwa
katika ripoti ya ubadhirifu, utapeli na wizi wa mali za chama hicho huenda
ikajulikana wiki ijayo baada ya vikao vya juu vilivyopangwa kufanyika
Jumatatu na Jumanne
Hatua hiyo ni baada ya mwenyekiti
wa CCM, Rais John Magufuli kuahidi kupeleka ripoti ya uchunguzi wa mali hizo
kwenye vikao hivyo ndani ya mwezi huu ili kuijadili na viongozi kutoa
maelekezo.
Taarifa ya chama hicho kwa vyombo vya habari
ilisema jana kuwa, kutakuwa na vikao vya Kamati Kuu (CC) pamoja na
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vitakavyofanyika kwa siku mbili, Mei 28 na 29
Hata hivyo, taarifa hiyo
iliyosainiwa na katibu wa NEC- Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole
ilisema kuwa vikao hivyo ni vya kawaida na kwamba vinaketi kwa mujibu wa
ibara ya 102(2) ya katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2017
Katika vikao hivyo, Polepole
alisema NEC pia itashughulika na kazi zake zingine, ikiwamo kujaza nafasi
zilizo wazi za wajumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa.
Kujazwa kwa nafasi hizo kunafuatia uchaguzi wa wajumbe wa NEC uliomalizika
Desemba 2017 ambapo wajumbe wanaoingia CC moja kwa moja kupitia nafasi zao
walishapatikana
Wajumbe hao ni mwenyekiti, makamu
wenyeviti, wenyeviti wa jumuiya za chama (vijana, wazazi na wanawake),
wajumbe wa sekretarieti (katibu mkuu, naibu makatibu wakuu na makatibu wa
itikadi na uenezi; fedha na uchumi; mipango na oganaizesheni na mambo ya
nje), maspika wa bunge, baraza la wawakilishi na waziri mkuu
Kutokana na uamuzi wa chama hicho
kupunguza idadi ya wajumbe kutoka 34 hadi 24, hivyo wajumbe wanaosalia
kukamilisha idadi ni wanane
Waliotajwa na kamati ya Bashiru
Wakati ikiwa ni wazi kuwa hatima
ya watu waliotajwa kwenye kamati iliyochunguza wizi, utapeli na ubadhirifu wa
mali za chama hicho huenda ikajulikana, wachunguzi wa masuala wa siasa
wanasema uwezekano wake ni mdogo kutokana na muda mfupi wa vikao hivyo
Hatua hiyo inafuatia ripoti ya
kamati ya kuhakiki mali za chama hicho iliyoundwa na Rais Magufuli chini ya
Dk Bashiru Ally kubaini upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa na
mikataba mibaya, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na
ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama
Akizungumza wakati wa kupokea
ripoti hiyo mapema wiki hii, Rais Magufuli ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM
alisema haiwezekani kupiga vita rushwa na ufisadi ndani ya Serikali wakati
chama kina rushwa na ufisadi
Alisema anataka pia chama
kisafishwe ili mambo ya rushwa na ufisadi yaishe na Tanzania iende vizuri
Rais Magufuli alienda mbali zaidi
na kuwaagiza wajumbe wa sekretarieti ya CCM waliohudhuria hafla ya
uwasilishwaji wa ripoti hiyo kuanza kufanyia kazi baadhi ya mambo yaliyo
ndani ya uwezo wao na kwamba, masuala mengine yataamuliwa na vikao vya juu
vya chama
Akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM jijini
Dodoma mwanzoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli aliwaambia wajumbe wa mkutano
huo kuwa anataka kusimamia mali za chama na chini ya uongozi wake chama hicho
hakitakuwa ombaomba tena
Alisema kwa miaka yote CCM imekuwa
ikiomba hata kwa watu ambao hawastahili wakati ina mali nyingi ambazo
zinatumiwa vibaya na baadhi ya wanachama ambao sio waaminifu
Kamati ya Dk Bashiru ilitangazwa
Desemba 20 mwaka jana ikiwa na wajumbe tisa
Akikabidhi ripoti hiyo, Dk Bashiru
alisema uhakiki huo umefanywa kwa mali za chama hicho, jumuiya na kampuni
zake
Alisema wakati wa utekelezaji wa
kazi hiyo, walitembelea maeneo yenye mali za chama hicho na kuwahoji watu
mbalimbali wakiwamo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa
Dk Bashiru alisema kuwa, kamati
imepitia nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika,
kufanya uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo
Maoni ya wachambuzi
Akizungumzia vikao hivyo, mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Beson Bana alisema hatua ya
kufikisha ripoti hiyo katika vikao vya juu vya chama hicho ni sawa, ingawa
haoni hatua kubwa itakayofikiwa kwa sasa kutokana na muda wa vikao kuwa mdogo
“Huwezi kumhukumu mtu bila kumpa
nafasi, vikao hivi vinakutana kwa siku mojamoja sidhani kama watapata nafasi
ya kuisoma ripoti hiyo yenye volume nyingi vile nilivyoviona na wakati huohuo
itoe haki sawa ya kuwasikiliza watuhumiwa kisha kutoa maamuzi,” alisema
Hata hivyo, Dk Bana alisema
dhamira ya Rais imeonekana wazi kwamba ana nia ya dhati ya kupinga ufisadi na
hata katika matukio mengine kama vile ya makinikia, wafanyakazi hewa na
walioghushi vyeti hakuchukua hatua mpaka pale alipounda tume kuchunguza
masuala hayo
“Nia ya dhati ipo ila wanahitaji
muda zaidi. Kwanza wajumbe wenyewe wanapaswa waisome ripoti ile kwa uangalifu
mkubwa kisha waliotuhumiwa wapate haki ya kujitetea kabla ya kuwachukulia
hatua, kwani naamini hilo limefanyika katika tume hiyo vivyo hivyo inapaswa
kufanywa na chama pia,” alisema Dk Bana
Hatua zaidi
Mwishoni mwa mwaka jana chama
hicho kilitangaza ‘kiama’ kwa wanachama wake waliojimilikisha mali za chama
hicho
Katika mahojiano maalumu na
Mwananchi, Polepole alisema kwa muda mrefu mali za chama hicho zilikuwa
zikimilikiwa na vikundi au watu binafsi jambo lililosababisha kukikosesha
mapato
“Nawaambia wajiandae kuanzia wiki
ijayo tutaanza kubomoa nyumba za watu, yakiwamo maghorofa ambayo yalijengwa
katika viwanja vya chama kwani mpaka sasa tumeshinda kesi kadhaa ambazo
zinatutaka tuyarejeshe maeneo yetu
“Kuna watu walidhani hatutawafikia
katika zoezi hili ukweli ni kwamba hakuna jiwe litakalobaki bila kugeuzwa. Na
huu ni mwanzo tu maafa zaidi yanakuja,” alisisitiza Polepole
Alisema katika uhakiki huo pia
wameweza kurudisha jumla ya viwanja vya michezo 22 kati ya 33 na hatua zaidi
zinaendelea ili kuhakikisha mali zote za chama hicho zinarudishwa
|
|
Kiama waliotajwa mali za CCM kuanza Jumatatu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 24, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment