Tume ya kuhakiki mali za Chama Cha Mapinduzi (CCM),
iliyoundwa na Rais John Magufuli, imebaini madudu ukiwamo utapeli na usimamizi
mbaya wa mali hizo.
Kamati hiyo iliyoundwa na Rais
Magufuli kukagua mali za chama hicho, imefanya kazi hiyo kwa miezi mitano
ambapo imekusanya taarifa, kuhakiki na kuchambua taarifa na nyaraka zenye
maelezo kuhusu idadi, aina na hali ya mali zinazomilikiwa na kusimamiwa na
chama hicho.
Akikabidhi ripoti hiyo kwa Rais John
Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Dk. Bashiru
Ally, amesema tume yake pia ilibaini usimamizi mbovu wa mali za chama.
Akielezea namna tume hiyo
ilivyofanya kazi, Dk. Bashiru amesema pamoja na mambo mengine, tume iliangalia
vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za usimamizi wa mali, imekusanya
ushauri mbalimbali na kutoa mapendekezo ya mikakati na ushauri wa kusimamia
mali za chama.
Katika ripoti hiyo, Dk. Bashiru
ameeleza tume imebaini uwepo wa upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa
na mikataba mibovu, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na
ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama.
“Uhakiki huo umefanyika kwa
kutembelea maeneo yenye mali za chama, kuwahoji watu mbalimbali wakiwamo
viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa, upitiaji wa nyaraka na
kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa
taarifa na kutoa mapendekezo,” amesema.
Kwa upande wake Rais Magufuli
ameipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya na amesema ripoti hiyo
itawasilishwa katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kwa ajili
ya kufanyiwa uamuzi.
“Nilipokuwa nateua tume hii,
nilikuwa najua ugumu wa kazi, nilikuwa najua kuwa mtapata shida kwenda kuwahoji
watu licha ya kwamba niliwapa uhuru wa kumhoji mtu yeyote na mmefanya kazi
nzuri sana, kilichobaki sasa ni kuifanyia kazi” amesema Rais Magufuli.
Ripoti ya Ufisadi Mali za CCM Yatua kwa Rais Magufuli
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 21, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 21, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment