Magufuli aiomba Denmark kusaidia ujenzi wa barabara


Rais John Magufuli ameiomba Serikali ya Denmark kusaidia ujenzi wa kipande cha barabara ya kilomita 11 katika Mkoa wa Iringa ili kuwezesha malori kutopita katikati ya mji huo na kupunguza ajali zinazotokea

Rais Magufuli amesema hayo leo Mei 3 wakati akizindua barabara ya Iyovi – Iringa – Mafinga yenye urefu wa kilomita 218 iliyojengwa kwa mkopo nafuu kutoka serikali ya Denmark na kugharimu Sh283 bilioni

Amesema mpango huo ulikuwepo tangu alipokuwa wizara ya ujenzi na kufafanua kwamba malori yanayopita katikati ya mji wa Iringa yamekuwa yakisababisha ajali kwa wakati wa mji wa huo

“Nakuomba Balozi, hili mlichukue kama la urgent (haraka), mkitusaidia kama mkopo sisi tuko tayari, mkitupa kama grant (msaada) tutashukuru zaidi. Kwa hiyo tunaomba utufikishie hili, ikiwezekana barabara hiyo tutaiita Pamela Road,” amesema Rais Magufuli huku wananchi wakipiga makofi

Rais Magufuli amewataka wananchi wa Iringa kuitumia barabara ya Iyovi – Iringa – Mafinga kama fursa ya kujiongezea kipato na kukuza uchumi wao. Amesema barabara hiyo ni kiungo muhimu kwa shughuli za kiuchumi

Amesema miundombinu ya barabara ni muhimu pia kwa uchumi wa viwanda kwa sababu inarahisisha bidhaa zinazotengenezwa viwandani kusafirishwa kwa urahisi kwenda kwenye masoko mbalimbali nchini au nje ya nchi

Awali, Rais Magufuli alizindua kiwanda cha kutengeneza chakula cha kuku cha Silverland Tanzania Ltd mkoani humo na kuwapongeza viongozi wa mkoa huo kwa kuvutia uwekezaji wa viwanda na amepewa taarifa kwamba mpaka sasa mkoa huo una viwanda 2,963

“Kukamilika kwa barabara hii kutafungua fursa nyingi, sasa wananchi mtaweza kusafirisha mazao yenu kuleta kwenye kiwanda cha Silverland, nao wataweza kusafirisha chakula cha kuku kwenda sehemu mbalimbali. Ni jukumu letu kuwajengea mazingira wezeshi kibiashara,” amesema

Magufuli aiomba Denmark kusaidia ujenzi wa barabara Magufuli aiomba Denmark kusaidia ujenzi wa barabara Reviewed by KUSAGANEWS on May 03, 2018 Rating: 5

No comments: