KESI MAUAJI YA BILIONEA ERASTO MSUYA: Mshtakiwa akana kukiri kumfyatulia risasi Msuya


Mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa jana alijitetea kwa kuyakana vikali maelezo yake ya ungamo kwa mlinzi wa amani, ambayo yanadaiwa alikiri ndiye aliyemfyatulia risasi, Erasto Msuya

Mshtakiwa huyo alienda mbali na kudai kuwa alisaini maelezo hayo baada ya kuteswa na hajui kilichoandikwa na kwamba, hajui kutumia SMG zaidi ya kujua kutumia panga na shoka

Msuya aliuawa Agosti 7, 2013 saa 6:30 mchana katika eneo Mijohoroni wilayani Hai, baada ya kushambuliwa kwa risasi 22 za bunduki ya kivita aina ya SMG na wanaoshukiwa ni washtakiwa

Maelezo hayo ya ungamo (extra judicial statement) ya mshtakiwa huyo yaliandikwa Septemba 16, 2013 na hakimu mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Moshi, Ponsian Claud aliyekuwa shahidi wa 12

Katika maelezo hayo yaliyosomwa mahakamani, shahidi huyo alidai mshtakiwa aliyatoa kwa hiari na kwa ridhaa yake, akieleza alifika eneo la tukio na mshtakiwa wa sita, Sadick Jabir wakiwa na pikipiki

Mshtakiwa anadaiwa kumweleza mlinzi huyo wa amani kuwa, ndiye aliyefyatua risasi kwa kutumia bunduki aina ya SMG akishirikiana na mtu aliyemtaja kwa jina moja la Sharifu na kumuua Erasto.

 Katika maelezo hayo ya ungamo, mshtakiwa anadaiwa kueleza kwa hiari yake kuwa kwenye utekelezaji mauaji hayo, alishirikiana na watu wengine watatu ambao ni Sharifu, Mredii na Sadik

Ushahidi mahakamani
Hata hivyo, jana akitoa ushahidi wake wa kujitetea, mshtakiwa alidai alilazimika kutia saini maelezo hayo baada ya kuteswa ikiwamo kunyimwa chakula na kuunguzwa miguu kwa pasi ya umeme

Akiongozwa na wakili wake, Majura Magafu kutoa utetezi wake, mshtakiwa huyo alidai kukamatwa wilayani Kaliua mkoani Tabora Septemba 13, 2013 akiwa na mshtakiwa wa sita, Sadick Jabir

Alidai kuwa walikwenda huko kwa ajili ya shughuli za uchimbaji dhahabu na kwamba, walikamatwa wakiwa kwa mganga aitwaye Sheikh Khalid Samkamula ambaye ni shahidi wa tano.

 Mshtakiwa huyo alidai kuwa alikwenda kwa mganga huyo kupata baraka na mafanikio ya kimaisha na kukana kuwa, hawakwenda kutafuta dawa ili wasikamatwe na polisi.</p></div><div><p>

Alieleza kuwa baada ya kukamatwa na shahidi wa tisa, Inspekta Samwel Maimu akiwa na shahidi wa 10, Seleman Mwaipopo na shahidi wa 11, Sajini Atway Omary, waliwekwa mahabusu kituo cha Kaliua

Ilipofika saa 4:00 usiku, mshtakiwa anadai alitolewa mahabusu na Inspekta Samwel na kuingizwa katika chumba kimojawapo na kumtaka amweleze kuhusu tukio la mauaji ya Erasto Msuya

“Nilimwambia hakuna ninachojua na baada ya kumjibu hivyo, alibadilika na kuniambia nampotezea muda kwani kila kitu anakijua. Alimuagiza Atway aende kwenye gari na kurudi na pasi ya umeme,” aliiambia Mahakama hiyo mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo

Alidai kuwa pasi hiyo iliwekwa kwenye umeme na kuwashwa, Sajin Atway na Koplo Seleman walimshika miguu huku Inspekta Samwel akianza kumchoma kwenye miguu

Mshtakiwa huyo alidai siku iliyofuata kati ya saa nne na saa tano asubuhi, waliondoka kurejea Moshi na walifika siku inayofuata, hapo aliwekwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Moshi

“Ilipofika mchana Samwel alikuja kunitoa lock up (mahabusu) na kunipeleka kwenye chumba kimojawapo wakati huo akiwa na karatasi akiniambia hataki utani anataka nizisaini,” alidai mshtakiwa huyo na kuongeza

“Sikuweza kuzisaini. Samwel alitoka nje akaja na kifaa aina ya “plaizi” alianza kunimega maganda kwenye vile vidonda alivyonichoma wakati huo vikiwa vimejaa maji na usaha.”

 Alidai kuwa Septemba 17, 2013, Inspekta Samwel alimtoa mahabusu na kumweleza kuwa anampeleka kwa mkuu wake wa kazi na lazima akubaliane na bosi wake, vinginevyo kipigo kingeanza tena

“Tulifika katika jengo moja hapa Moshi mjini, Samwel aliingia katika hilo jengo akiwa na bahasha. Baada ya muda alitoka na kuwaamuru polisi aliokuwa nao waniingize ndani

“Huyo mkuu wake (Hakimu Claud) aliniuliza swali moja tu, kwamba wewe ni Karim Kihundwa? Nikamwambia ndiyo, akaniambia nataka unisainie hapa. Sikusomewa hizo karatasi,” alidai shahidi huyo na kuongeza

“Kutokana na hali yangu ya afya nilikuwa nimedhoofu sana kwa njaa na maumivu ya vidonda, nilisaini hizo karatasi. Huyo mkuu wake ndiyo ushahidi hapa akisema nilitoa maelezo ya ungamo.”

Akiongozwa na Magafu, mshtakiwa huyo alidai maelezo hayo hajawahi kuyatoa na siku ya mauaji ya Erasto Msuya Agosti 7, 2013 alikuwa shambani kwake West Kilimanjaro akivuna karoti

“Siyo kweli kwamba nilimweleza kuwa mimi ndiye niliyemfyatulia risasi na kumuua Erasto Msuya. Sijawahi kufanya hivyo wala hiyo tarehe sikuwapo na wala sijawahi kupitia mafunzo ya kijeshi,” alidai

Pia, alikanusha maelezo yaliyomo katika maelezo ya onyo ya kukiri kosa ya mshtakiwa wa kwanza, Sharifu; wa tatu, Mussa Mangu; na wa saba, Ally Majeshi kwamba walishiriki kumuua Msuya

“Niliiona hii bunduki ya SMG (kielelezo namba 13) kwa mara ya kwanza ilipotolewa hapa mahakamani. Sijawahi kumiliki bunduki wala sijawahi kutumia bunduki,” alidai mshtakiwa

Awali, katika ushahidi wake huo, alidai kuanzia Agosti 7, 2013 alikuwa shambani kwake West Kilimanjaro wilayani Siha na alirejea nyumbani kwake Bomang’ombe Agosti 10, 2013

Pia, alikanusha ushahidi wa shahidi wa 27 wa mashtaka, Inspekta Damian Chilumba aliyedai kwamba aliwapeleka yeye na Sadick kwa mkemia wa Serikali na kuwachukua sampuli za vinasaba (DNA

Akihojiwa na wakili Hudson Ndusyepo anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, Sharifu, mshtakiwa huyo alikana kumfahamu mshtakiwa huyo na wengine akieleza kuwa amekutana nao katika kesi hiyo

Akihojiwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavulla alimuuliza mshtakiwa huyo kama alikuwa anafahamu jengo lililopo upande wa pili wa barabara ni la Mahakama

Mshtakiwa huyo alijibu kuwa kabla ya kupatwa na misukosuko ya kesi hiyo alifahamu kuwa jengo hilo ni la Mahakama kwa vile wakati akipita na basi kwenda Moshi, alikuwa akikuta polisi wengi.

Alipoulizwa na wakili Chavulla kama ndilo jengo alilopelekwa na Inspekta Samwel kwa mtu aliyedai ni mkuu wake wa kazi, mshtakiwa huyo alidai si kweli kwamba aliwahi kupelekwa katika majengo hayo

Wakili huyo alimuuliza kama alisikia ushahidi wa shahidi wa 12 (mlinzi wa amani), akijitambulisha kuwa ni hakimu mkazi anayefanya kazi katika Mahakama ya Mwanzo Moshi, alikubali kusikia

Pia, alipotakiwa akubali kwamba alipelekwa katika majengo ya hakimu huyo na kuandika maelezo ya ungamo, mshtakiwa huyo alidai kama alipelekwa katika jengo hilo basi alipitishwa njia nyingine

Kuhusu kama alikuwa anafahamiana na hakimu aliyeandika maelezo yake ya ungamo au kuwa na ugomvi naye, mshtakiwa huyo alidai alikuwa hamfahamu na wala hakuwa na ugomvi naye

Aliulizwa kama polisi wanaweza kumuonea mtu, mshtakiwa huyo alidai inawezekana na kutolea mfano kuwa kuna askari Kituo cha Polisi Bomang’ombe aliwahi kumpeleka bila kuwa na kosa

Chavulla alimtaka aiambie Mahakama kabla ya kukamatwa alikuwa akifanya shughuli gani, mshtakiwa alidai kwamba alikuwa akimiliki salon tatu kwa jina la Gorilla zilizokuwa zikimuingizia Sh500,000 kwa mwezi

Kesi hiyo itaendelea leo kwa mshtakiwa wa sita, Sadick Jabir kuanza kujitetea

KESI MAUAJI YA BILIONEA ERASTO MSUYA: Mshtakiwa akana kukiri kumfyatulia risasi Msuya KESI MAUAJI YA BILIONEA ERASTO MSUYA: Mshtakiwa akana kukiri kumfyatulia risasi Msuya Reviewed by KUSAGANEWS on May 17, 2018 Rating: 5

No comments: