Jinsi kijana aliyeokolewa Z’bar alivyoingia ndani ya kontena

Siku moja baada ya mkazi mmoja wa Miembeni Unguja kutolewa ndani ya kontena alimokaa kwa siku tatu, polisi imesimulia kilichojiri hadi kujikuta katika hali hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassri Ali akizungumza na Mwananchi jana alisema kwa mujibu wa mahojiano na kijana huyo anayeitwa Hassan Juma Hassan (36), aliingia ndani ya kontena lililokuwa Bandari ya Malindi kujikinga na mvua

Alisema kijana huyo alitokea baharini anakojishughulisha na uvuvi na alipofika eneo yanakoegeshwa makontena yaliyoshusha mizigo, aliamua kuingia ndani ya mojawapo akisubiri mvua ikatike
Kamanda Nassir alisema wakati mvua ikiendelea kunyesha, kontena lilihamishwa lilipokuwa na kupandishwa juu

Wakati hilo likifanyika, kamanda alisema kijana huyo alipiga kelele, lakini waliokuwa wakilihamisha hawakusikia

“Kutokana na kupata mtikisiko akiwa ndani ya kontena lililobebwa kupandishwa juu inaonekana alipoteza nguvu hata hakuweza kuita tena. Ndipo alipokaa humo kwa siku tatu bila ya kula hata kunywa,” alisema Kamanda Nassir akinukuu mahojiano ya kijana huyo na Jeshi la Polisi.

 Kamanda Nassir alisema baada ya siku tatu ndipo alipopata fahamu na kupiga kelele akigonga kontena hatimaye walinzi na watu waliokuwa eneo hilo walisikia sauti na kumtoa

Kamanda Nassir alisema baada ya mahojiano, kijana huyo ameruhusiwa kurudi nyumbani kuendelea na shughuli zake.
Msemaji mkuu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar, Hassan Makame alisema afya ya kijana huyo aliyefikishwa hospitalini hapo juzi, inaendelea vizuri

Jinsi kijana aliyeokolewa Z’bar alivyoingia ndani ya kontena Jinsi kijana aliyeokolewa Z’bar alivyoingia ndani ya kontena Reviewed by KUSAGANEWS on May 15, 2018 Rating: 5

No comments: