Mshtakiwa katika kesi ya kujiteka na
kusambaza taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii, Abdul Nondo ameandika
barua ya kumkataa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Iringa, John Mpitanjia,
anayesikiliza kesi hiyo kwa madai ya kuwa karibu na Mkuu wa Upelelezi
wa Polisi Mkoa wa Iringa.
Wakili anayemtetea Nondo,
Jebra Kambole ametoa sababu tano za mteja wake kuandika barua hiyo tangu
Mei 11, mwaka huu za kumkataa hakimu huyo ikiwamo hakimu huyo kuonekana
akiingia katika gari la Mkuu wa Upelelezi na kwenda sehemu isiyojulikana,
ambapo kutokana na hali hiyo, mteja wake ameona haki haitatendeka.
Amedai sababu nyingine ni hakimu
huyo kukutwa amekaa na Paul Kisapo ambae ni shahidi wa tatu katika kesi hiyo.
Kwa upande wake Wakili Upande wa
Jamhuri, Abel Mwandalama amedai pamoja na kupokea barua ya mshtakiwa
kumkataa hakimu lakini ameona hayana msingi katika kesi hiyo.
“Tunasema hayo kwa kuwa Aprili 19,
shahidi wa tatu katika shauri hilo alitoa ushahidi wake na
mshitakiwa hakuandika barua yoyote na hata kesi hiyo ilipokuja tena Mei
10, mwaka huu hakuna barua iliyoandikwa iweje barua hiyo kuandikwa Mei
11, baada ya mahakama hiyo kukubali vielelezo vilivyotolewa na upande wa
jamhuri kutumika kama ushahidi,” amedai Wakili Mwandalama.
Baada ya kusikiliza hoja za pande
zote mbili, Hakimu Mpitanjia alisema uamuzi wa kujitoa ama kuendelea na kesi
hiyo utatolewa Mei 16, mwaka huu.
Nondo anakabiliwa na mashtaka mawili
ambayo ni kusambaza taarifa za uongo akiwa Ubungo jijini Dar es Salaam, na
kutoa taarifa za uongo akiwa mjini Mafinga kwa askari Polisi kituo cha Mafinga
Wilayani Mufindi.
Abdul Nondo Amkataa Hakimu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 14, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment