Watu 228,000 wahitaji dawa, chakula Kenya


Baadhi ya maeneo yamefunikwa na maji Kenya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini humo huku zaidi ya watu 228,000 wakihitaji msaada maalumu ikiwamo chakula na dawa.

Mvua hizo zimesababisha vifo, maporomoko ya ardhi na uharibifu wa miundombinu kwa kiasi kikubwa pembe nyingi za nchi hiyo yamesababisha idadi kubwa ya wananchi kukosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kubomoka.

Katika kaunti ya Tana River, Gavana Dhadho Godhana alisema asilimia 70 ya wakazi wameathiriwa huku watu 11 wakidaiwa kupoteza maisha kwa kusombwa na mafuriko.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi, Gavana Dhadho alisema miongoni mwa waliopoteza maisha ni pamoja na watoto wadogo.

Gavana huyo alisema mbali na Mto Tana kuvunja kingo zake, mito mingine midogo inayoanzia kaunti za Kitui na Makueni imejaa maji na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na watu kupoteza maisha.

“Katika baadhi ya maeneo watu wanaishi katika kambi 106. Familia 38,000 zimeathiriwa moja kwa moja na mafuriko,” aliongeza Gavana Dhadho.

Alisema watu 228,000 wanakabiliwa na hatari ya kupata maradhi, hawana makazi, chakula, dawa, maji safi na mahitaji mengine.

“Watu wanaoishi kando ya Mto Tana wanakabiliwa na tisho kuu la njaa baada mimea yao kuharibiwa na mafuriko,” alisema.

Hali ya uchukuzi pia imeathiriwa na misaada inaweza kupelekwa kwa ndege au kwa mashua.

Gavana Dhadho alitoa wito kwa mashirika ya kutoa misaada kujitokeza kuungana na Serikali yake kusaidia waathiriwa.

Kamishna wa kaunti hiyo Michael Kioni alisema kaunti ndogo ya Tana Kaskazini ndiyo imeathirika sana, familia 16,000 zimeathirika ikifuatiwa na ile ya Tana Delta ambapo familia 14,000 zimeathirika.  Kaunti ndogo ya Tana River ni ya tatu ambayo ina waathiriwa 8,000.

Wakati huohuo watu nane walikufa baada ya kusombwa na mafuriko katika matukio tofauti Kaunti ya Kisii kufuatia mvua hiyo  inayoendelea kunyesha kote nchini.

Mtu mmoja  alisombwa na maji katika eneo la Nyambunde, Kaunti ndogo ya Bobasi alipokuwa akivuka daraja kwenye Mto Gucha uliofurika.

Katika eneo la Ogembo, watu wawili walipoteza maisha baada ya kusombwa na maji walipokuwa wakijaribu kuvuka mto huo.

Mvua hiyo ilisababisha uharibifu mkubwa kwenye mashamba huku nyumba zilizokuwa karibu na mto huo zikiharibiwa pia.

Eneo la Daraja Mbili, mjini Kisii watu wengine walikufa maji baada ya kujaribu kuvuka daraja na kusombwa na Mto Nyakomisaro.

Watu zaidi ya 100 kutoka maeneo ya Mugirango Kusini na Bobasi, hawana makazi baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko.

Msimamizi wa Idara ya Majanga katika Kaunti ya Kisii Dk Walter Okib alisema kuwa mvua hiyo imesababisha hasara katika maeneo hayo na kusababisha vifo kadhaa.<
Watu 228,000 wahitaji dawa, chakula Kenya Watu 228,000 wahitaji dawa, chakula Kenya Reviewed by KUSAGANEWS on April 30, 2018 Rating: 5

No comments: