Spika wa Bunge la Afrika Mashariki
(EALA), Dkt. Martin Ngoga ameishukuru na kuipongeza Serikari ya Tanzania kwa
ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo wa reli kwa sababu inaleta
manufaa hata kwa nchi jirani.
“Miradi hiyo ambayo kwa sasa inatekelezwa
kwa kasi si kwamba inachochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania, bali hata wa nchi
nyingi za jirani kwa kuwa nazo zitanufaika na miradi hiyo kwani si nchi zote
zina bandari”.
Dkt. Ngoga ameyasema hayo leo
(Jumatatu, Aprili 23, 2018) alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa, Bungeni mjini Dodoma.
Amesema tayari wamejadili ripoti
iliyotokana na ziara iliyofanywa na wabunge hao katika upande wa korido ya
kuishi na korido ya kaskazini ambapo wametoa mapendekezo yatakayofanyiwa kazi
na baraza la mawaziri.
“Tayari tumeshajadili miswada miwili
inayohusu Itifaki ya Sarafu Moja ambayo ni mswada wa taasisi ya Fedha na
mswada wa Takwimu yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2017.”
Pia Spika huyo amesema wamefurahia
uwepo wao nchini, ambapo mbali na shughuli zao za kibunge pia kwa kushirikiana
na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wameshiriki kampeni ya kukijanisha Dodoma
kwa kupanda miti 1,000 kwenye eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Kwa upande wake, Waziri Mkuu amesema
amefarijika na uamuzi wa Bunge la EALA kufanya vikao vyake katika nchi
wanachama kwa sababu unatoa fursa ya kujua mazingira ya nchi hizo pamoja na
maendeleo yake.
Amesema nchi wanachama wanamatumaini
makubwa na bunge hilo katika kuimarisha na kuboresha maendeleo ya mataifa
yao, hivyo amewatakia mjadala mwema.
Katika hata nyingine, Waziri Mkuu
amewakaribisha wabunge hao na marafiki zao kuja kuwekeza kwenye sekta
mbalimbali nchini ikiwemo ya viwanja, utalii, kilimo na madini.
Kwa mara ya kwanza vikao vya Bunge
la Afrika Mashariki, (EALA) vinafanyika Dodoma katika ukumbi wa Bunge wa Msekwa
ulipo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vikao hivyo vilianza
Aprili 17, 2018 na vinatarajiwa kumalizika Aprili 29, 2018.
Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Aipongeza Tanzania Kwa Maendeleo
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 23, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment