Majaji wapya watakiwa kufuata sheria



Majaji wapya walioapishwa mbali ya kuhimizwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, wametakiwa kuzisoma na kuzitafsiri vyema sheria kwani kama watafanya vinginevyo wanaweza kuipoteza nchi
Kamishna wa Maadili, Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Harold Nsekela amewaambia majaji hao leo Ijumaa Aprili 20 Ikulu kuwa kazi waliyopewa inahitaji umakini na uadilifu

“Someni sheria na kuzitafsiri vizuri... Mahakama ndiyo chombo pekee kinachotafsiri sheria na kama mtatafsiri vibaya mnaweza kuipoteza nchi,” amesema jaji huyo wakati akitoa nasaha zake baada ya majaji hao wapya kuapishwa na Rais John Magufuli

Alisisitiza kuwa katika utendaji wa kazi kumekuwa na mgawanyiko wa majukumu wakati Bunge likitunga sheria, Serikali kazi yake kubwa ni kupendekeza sheria hizo

“Mahakama ndiyo inayotoa tafsiri hivyo ili kuifanya vyema kazi hiyo lazima mtapaswa kusoma sana na someni kwa makini maana kile mnachokiamua nyinyi ndiyo mwongozo wa mwisho mpaka pale Bunge litakapoamua kutunga sheria nyingine,” amesema

Kuhusu kuishi kwa uadilifu kamishna huyo aliwataka majaji hao kujichunguza mienendo mibovu itakayoweza kuwaondoelea heshima kwa jamii

 “Chagueni vyema marafiki zenu ikiwezekana achaneni na wale wanaoonekana kutokuwa wema... na ikiwezekana ukitoka zao kazini nenda nyumbani na siku kama ya leo Ijumaa nenda msikitini kwa wale Waislamu na wale Wakristo nendeni kanisani Jumapili ... mnaweza kwenda pia kwenye burudani lakini angalieni burudani mnazokwenda,” amesema

Rais Magufuli leo amewaapisha majaji wapya kumi, wakili mkuu wa serikali na naibu wake na naibu mkurugenzi wa mashtaka
Sherehe za kuwaapisha majaji hao zinafanyika Ikulu na zinahudhuriwa na wageni mbalimbali akiwamo Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma.
Majaji wapya watakiwa kufuata sheria Majaji wapya watakiwa kufuata sheria Reviewed by KUSAGANEWS on April 20, 2018 Rating: 5

No comments: