Askari doria uvuvi haramu wachongewa kwa DC


Askari wanaoshiriki doria kuzuia uvuvi haramu wilayani Sengerema, wamedaiwa kuwakamata na kuwapiga wananchi wakiwamo wanafunzi wakiwashinikiza kuonyesha zilikofichwa zana haramu.

Tuhuma hizo zilitolewa juzi na wananchi wakiongozwa na diwani wa Kahumulo, Mashauri Nzwagi wakati wa kikao cha pamoja kilichoitishwa na mkuu wa wilaya hiyo, Emmanuel Kipole kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wafanyabishara wa samaki, wavuvi, wananchi na maofisa wanaoshiriki doria hizo. “Hawa maofisa wanaoshiriki doria wanawakamata na kuwapiga hovyo wananchi bila sababu za msingi. Wapo wananchi wameumizwa,” alisema Nzwagi.

Aliwataja wanafunzi wawili ndugu wa Sekondari ya Kahumulo, Kelvin Zambona na Mzilya Zambona kuwa ni miongoni mwa waliopigwa na kujeruhiwa na askari hao wa doria waliokutwa wakitoka tuisheni.

Wakitoa ushuhuda, wanafunzi hao walisema askari hao waliwakamata saa 11:00 jioni ya Aprili 22, wakiwa njiani wakitoka shule na kuwataka waonyeshe baba yao alikofichwa zana haramu za uvuvi.

“Baada kuwajibu kuwa baba yetu hana zana haramu za uvuvi, wala hatujui kama anashiriki vitnedo hivyo, ghafla askari likaanza kutupiga,” alisema Kelvin.

Naye mkuu wa kikosi cha doria wilayani Sengerema kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wenceslaus Luhasile aliahidi kuchunguza tuhuma hizo na kuonya kuwa hatua za kisheria na nidhamu zitachukuliwa iwapo itathibitika kuwa askari hao wamehusika na vitendo vinavyokiuka sheria.
Askari doria uvuvi haramu wachongewa kwa DC Askari doria uvuvi haramu wachongewa kwa DC Reviewed by KUSAGANEWS on April 30, 2018 Rating: 5

No comments: