ACT wamwandikia barua IGP

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimesema kimepokea taarifa katika mitandao ya kijamii kuhusu tishio la kuuawa kwa Kiongozi wake, Zitto Kabwe

Katibu wa Itikadi, Mawasiliano kwa Umma na Uenezi, Ado Shaibu amesema taarifa hizo hawakuzipuuza na tayari chama kimemuongezea ulinzi Zitto, ili kukabiliana na tishio hilo

Kauli hiyo ameitoa leo Aprili 23, 2018 wakati wa mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam

"Lakini tumemwandikia barua IGP ili achunguze taarifa hizo, hatuwezi kupuuza kwa sababu Chadema ililalamika kabla ya shambulio la Tundu Lissu, hatupuuzi kwa sababu, leo hii hatujui Ben Saanane yuko wapi," amesema Shaibu.

Katika hatua nyingine, Shaibu amesema ACT imebaini udanganyifu wa Serikali katika ufafanuzi wa sakata la Sh1.5 trilioni

Amesema baada ya kuchunguza, ACT kimebaini akaunti ya Zanzibar pamoja na Hesabu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mwaka unaoishia Juni 30 mwaka jana, hazionyeshi taarifa ya Sh203 bilioni kupelekwa Zanzibar

Ufafanuzi bungeni wiki iliyopita, naibu waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashantu Kijaji alitaja maeneo matatu ya kutumika kwa Sh1.5 trilioni, akisema kati ya fedha hizo Sh203 bilioni zilikuwa ni makusanyo ya kodi kwa ajili ya Serikali ya Zanzibar



ACT wamwandikia barua IGP ACT wamwandikia barua IGP Reviewed by KUSAGANEWS on April 24, 2018 Rating: 5

No comments: