Imeelezwa kuwa
matatizo ya kisaikolojia yanayoendana na msongo wa mawazo yanayowakumba zaidi
wanaume chini ya umri wa miaka 35, yamekuwa chanzo cha kuwepo kwa upungufu wa
nguvu za kiume.
Hata hivyo
madaktari wameonya kwamba kila tatizo lina chanzo chake, hivyo si sahihi kwa
mwathirika kujitibia kwa dawa yoyote kabla ya kuonana na wataalamu ili kujua
kisababishi na kutibu tatizo husika.
Akizungumza na
Mwananchi, Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo, Obadia Nyongole
anasema upungufu wa nguvu za kiume una sababu tofauti
“Watu wanachanganya
kati ya upungufu wa nguvu za kiume na kukosa hamu ya tendo la ndoa hivyo ni
vitu viwili tofauti, mwanaume anaweza akawa na nguvu za kiume lakini anakosa
hamu ya tendo la ndoa,” anasema.
Daktari bingwa
wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro
Pallangyo ameeleza kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wanasumbuliwa na tatizo kubwa
la shinikizo la damu na kisukari, wengi wao wanapungukiwa nguvu za kiume
”Hali hii
inaashiria kuwa magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu yamekuwa yakiongezeka
mara kwa mara jambo ambalo linasababisha athari ya nguvu za kiume kuwa kubwa,”
anasema Dk Pallangyo.
Dk Nyongole
ambaye pia ni Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) anasema kwamba zipo aina
mbili za kukosa nguvu za kiume ipo inayotokana na matatizo mbalimbali ya
kimwili ambayo husababishwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo homoni ambazo
husababisha wengine kuwa na homoni za kike.
Anasema wapo
wanaokuwa na ukosefu wa nguvu za kiume kutokana na matatizo ya kiafya yaliyopo
kwenye miili yao na wapo ambao wanakuwa na ukosefu wa nguvu za kiume kutokana
na matatizo ya kisaikolojia ikiwemo msongo wa mawazo
“Kwa hili la
ukosefu wa nguvu za kiume linalotokana na matatizo ya kisaikolojia au
yanayoendana na msongo wa mawazo hili linawakumba zaidi wanaume hasa wale walio
chini ya umri wa miaka 35
“Haimaanishi
kwamba linaweza kuwakumba wanaume wenye huo umri pekee, ila waliopo kwenye umri
wa kuzaa mwingine anakuwa na msongo wa mawazo labda hana mahusiano mazuri
kwenye ndoa yake au kazi inamkosesha hamu ya tendo la ndoa hivyo inapunguza
nguvu za kiume.”
Dk Nyongole
anasema kwamba tatizo hilo huwakuta zaidi watu ambao bado ni vijana lakini
hawana magonjwa mengine ya kimwili zaidi ya yale ya kisaikolojia
“Mara nyingi
utakuta labda mahusiano yaliyopo kwenye ndoa hayamridhishi, kubadilika kwa
mfumo wa maisha, walikuwa wanaheshimiana sasa heshima hakuna, mama alikuwa
anajiweka vizuri lakini sasa hivi hajiweki vizuri, mfano anaweza akasikia
harufu ya ‘perfume’ kwa mwenzake lakini asiipende, basi hamu inamuisha kabisa.”
Anasema kwamba
kuna wakati mmoja kati yao akahitaji zaidi lakini kimazingira hawajaandaana
vizuri, “Mama akisema siku hizi huniridhishi basi anapata wasiwasi na msongo wa
mawazo unaingia baada ya hapo anakuja kumaliza haraka kwa sababu anafanya kwa
ajili ya kufanya na si kwamba anafurahia tendo.”
Hata hivyo
anaongeza kwamba kuna ukosefu wa nguvu za kiume unaotokana na magonjwa
mbalimbali ikiwemo matatizo ya kiafya kama kisukari, presha, magonjwa ya figo
au mhusika alishawahi kupata ajali inayohusisha maungo ya uume.
Anasema wakati
mwingine mwanaume anaweza kuwa na matatizo ya magonjwa yanayohusisha madhara ya
kwenye mishipa midogomidogo ya kwenye damu inayosababisha uume usiweze kusimama
vizuri akafanya tendo la ndoa vizuri
“Wapo wengine
ambao wana matatizo ya magonjwa ya moyo yanayofanya mishipa ya damu ijae mafuta
zaidi na kuathiri mzunguko wa damu au ana dawa anazotumia za presha kisukari
zinazomletea hayo matatizo na mwingine ana matatizo ya ukosefu wa nguvu za
kiume kutokana na magonjwa au dawa anazotumia,” anasema
Utafiti Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine
Ndugulile anasema Serikali imeamua kufanya utafiti wa tatizo la ukosefu wa
nguvu za kiume kwa wanaume kwa sababu kwa muda mrefu wamekuwa wakitafuta
suluhisho kwa kificho na hivyo kukosa taarifa sahihi.
Dk Ndugulile
amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulisubisya kushirikiana na
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kufanya utafiti wa
afya ya uzazi kwa wanaume ili kubaini sababu ya ongezeko la upungufu wa nguvu
za kiume ni kubwa kwa kiasi gani nchini.
Hata hivyo
anasema kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikitilia mkazo afya ya uzazi kwa
wanawake na tafiti nyingi zimekuwa zikihusu upande huo mmoja.
Alisema mpaka
sasa bado haujafanyika utafiti kuhusu hali ya afya ya uzazi kwa wanaume, japo
tatizo hilo linazungumzwa miongoni mwa wanajamii
“Bado
hatujafanya utafiti wa kina kujua tatizo hili ni kubwa kwa kiasi gani, suala
hili ni gumu kulisemea kwa maana ukiangalia takwimu ya uzazi Tanzania kwa maana
ya ongezeko la watu na idadi ya kinamama kukua unaona kabisa kwamba bado hatuna
shida,” anasema na kuongeza
“Tatizo hili
sisi wenyewe tunachangia kwa kula bora chakula na si chakula bora hasa vyakula
vyenye mafuta kwa wingi, sukari vinachangia sana katika magonjwa yasiyo ya
kuambukiza pamoja na kupungua kwa nguvu za kiume, kutofanya mazoezi, matumizi
ya vilevi ikiwemo pombe na sigara navyo ni visababishi vikuu,” anasema Dk
Ndugulile
Kufuatia hilo,
Dk Nyongole anasema kwa Serikali kuamua kulifanyia utafiti tatizo hilo,
kutaibua tiba maalum kwani nchi itajua hasa nini kiini cha tatizo hilo
“Ni suala zuri
kwa sasa lakini ni namna tu ya kujua kwamba wanatarajia utafiti huu ufanyike
kwa njia gani na kwa wakati gani na baada ya muda gani au lini tutarajie
majibu,” anasema na kuongeza, “baada ya majibu sisi kama wataalamu tutakuja na
kusema kilichoonekana kinamaanisha nini na nini kifanyike.”
Mapema wiki
hii Serikali imetangaza rasmi kuzitambua aina tano za dawa za asili baada ya
kuzikagua ikiwemo ‘Ujana’ inayodaiwa kutibu nguvu za kiume
Dawa hizo
zilizotangazwa juzi kupitia mkutano wa vyombo vya habari, zimetajwa kuwa ni
Ujana, IH Moon, Coloidal Silver, Sudhi na Vatari.
Msemaji wa
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Gaudensia Simwaza alisema hadi sasa dawa
ambazo zimesajiliwa na mamlaka hiyo baada ya kuchunguzwa na kuonekana zinafaa
kutumiwa na binadamu ni aina mbili
“Kuna dawa
aina mbalimbali zikiwemo Sildenafil pamoja na tadalafil zinazotoka nchi
mbalimbali ambazo zimechunguzwa na TFDA na kuonekana hazina sumu wala madhara
kwa watumiaji, hizi zinapatikana katika maduka mbalimbali ya dawa za binadamu,”
alisema Simwaza.
Upungufu nguvu za kiume tishio kwa vijana chini ya miaka 35
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 21, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment