Serikali imewapiga marufuku wanaume
wanaotumia mali za familia kama dhamana za mikopo bila kuwashirikisha wake zao
kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria, kanuni na taratibu za ndoa nchini.
Hayo yamesemwa na Mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa Wilaya
ya Arusha, Fabian Daqarro kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid wakati wa
maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani .
Daqarro amesema kuwa wapo wanaume wanaotumia
mali za familia kama nyumba kukopa bila kuwashirikisha wake zao na wakishindwa
kulipa mikopo, mali ya familia hupigwa mnada
“Niwakaribishe kwangu mje mtoe taarifa
endapo ukigundua mume wako amechukua mkopo na kuweka dhamana mali ya familia
kati ya nyumba, gari, shamba au chochote nawaahidi nitasema nao kwa mujibu wa
sheria maana ndio wanaotujengea wingi wa watu tegemezi baadae,” amesema.
Mbali na hilo amewataka wanawake kuwa mstari
wa mbele katika kupinga ukatili wa kijinsia na mila potofu hasa za umiliki wa
ardhi na mali za familia lakini pia kuungana kwa pamoja
“Nguvu ya kutokomeza ukatili na unyanyasaji
wa kijinsia iko mikononi mwenu wanawake kwa kupendana na kuacha husuda na chuki
za waziwazi baina yenu, badala yake muwezeshane maana mafanikio ni kumiliki
uchumi lakini pia kupendana kwani wengine wanaotekeleza ukatili huu kwa
mwanamke ni wanamke wenyewe,” amesema Daqarro na kuongeza
“Ukomavu wa kumiliki uchumi ndio nguvu
ya mwanamke na silaha pekee ya kupinga ukatili hivyo wajengeeni watoto
wenu wa kike hili tangu wadogo huku mkiwapa elimu maana ndio nguzo kuu ya
familia na jamii, mkitimiza haya yote basi ukatili na unyanyasaji mtakuwa
mmeutokomeza maana hamtakuwa mnategemea kuwezeshwa bali kuwezesha.”
Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa Jiji
la Arusha, Athumani Kihamia amesema kuwa zaidi ya vikundi 110 vya wanawake
vimewezeshwa mikopo ya zaidi ya Sh2 bilioni kwa lengo la kuwapa fursa ya
kutekeleza nchi ya viwanda katika vikundi vya ujasiriamali.
Serikali yapiga marufuku wanaume wanaotumia mali za familia kama dhamana ya mikopo
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 08, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment